MITAZAMO YA JAMII KUHUSU PAROLE

Fikra: Jukumu la kushughulika na watu waliovunja Sheria ni la Serikali pekee.
Ukweli: Serikali ni chombo cha jamii kinachosimamia Sheria na Kanuni zilizowekwa na kukubalika katika jamii husika. Utekelezaji wa majukumu ya msingi ni wajibu wa jamii nzima. Aidha, wanaovunja Sheria ni wanajamii ambao Serikali kama chombo cha usimamizi, kupitia Jeshi la Magereza ina jukumu la msingi katika kuwarekebisha ili warudi kwenye jamii walizotoka wakaishi kama raia wema.

Mchakato wa urekebishaji wa wahalifu hauwezi kukamilika Gerezani. Usemi kuwa mgonjwa haponi kabisa akiwa hospitalini ni wa kweli. Hospitalini mgonjwa hufanyiwa uchunguzi na kupatiwa huduma stahiki za matibabu. Kisha kurejea kwenye familia ili familia na jamii wakishirikiana na madaktari waendelee kumfariji na kumpa huduma zitakazomwezesha kurejea katika afya yake kamili. Hali kadhalika mchakato wa urekebishaji wa wahalifu hauwezi kukamilika pasipo Jeshi la Magereza kuzishirikisha familia zao, jamii zao na wadau wengine katika kuwasaidia wahalifu wabadili tabia na kuishi kama raia wema. Utaratibu pekee wenye uwezo huo ambao unakubalika kisheria ni Parole. Ili jamii iweze kuwasaidia kikamilifu, jamii inapaswa kubadili mtazamo (attitude) iepuke kuwakataa, kuwatenga na kuwanyanyapaa.


Fikra: Wafungwa  wa Parole wanapokuwa kwenye jamii hurudia kutenda makosa.
Ukweli: Wafungwa wa Parole walio wengi hawarudii makosa wala kutenda makosa mapya wakiwa wanatumikia vifungo chini ya Parole. Tangu kuanzishwa kwa Parole mpaka sasa wafungwa waliorudishwa gerezani kwa makosa mbalimbali ni 1.3% tu.


Fikra: Parole hutolewa kwa kila mfungwa aliyehukumiwa mara tu anapokuwa ametumikia 1/3 ya kifungo chake.
Ukweli: Sheria ya Parole imeainisha sifa za wafungwa wanaostahili kunufaika na Parole. Pamoja na sifa anazotakiwa kuwa nazo mfungwa anayeomba kunufaika na mpango wa Parole, usalama wa jamii na mfungwa ni vigezo muhimu sana kabla ya kumpitisha mfungwa husika kunufaika na Parole. Hivyo kabla ya kuanza kujadiliwa, Jeshi la Magereza hujiridhisha na kiwango cha kujirekebisha kwa mfungwa pamoja na kuiandaa familia na jamii kumkubali na kumpokea ili atakapopata fursa ya kwenda kujiunga na jamii asiweze kuleta madhara katika jamii na pia awe anakubalika na jamii husika ikiwa ni pamoja na mwathirika wa tukio.

Fikra: Parole hupunguza urefu wa kifungo alichohukumiwa mfungwa.
Ukweli:  Parole inamruhusu mfungwa kutumikia sehemu ya kifungo chake kilichobakia akiwa kwenye jamii chini ya uangalizi na masharti maalum. Anapokiuka masharti hayo anaweza kurudishwa gerezani kwa uamuzi wa mahakama/kwa kuihusisha mahakama.


Fikra: Mfungwa anaponufaika na Parole ana uhuru wa kuishi anavyotaka.
Ukweli: Mfungwa wa Parole lazima aishi kwa kufuata Sheria na masharti aliyopangiwa. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum, kutoondoka katika sehemu aliyokubaliwa kuishi chini ya Parole bila kibali na kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka muda wake wa kifungo utakapomalizika.

.