Na Lucas Mboje, Njombe

WAKUU wa Magereza yote nchini wametakiwa kuwa wabunifu ili kutatua changamoto ya uhaba wa makazi ya askari kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa na rasilimali nyinginezo zilizopo katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa leo Novemba 12, 2018 na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua magereza yote ya Mkoa wa Njombe ambayo yanaendeshwa na Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa lazima wakuu wa magereza wawe wabunifu katika kutatua tatizo hilo la uhaba wa nyumba kwani Jeshi hilo linazo fursa nyingi ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa.

“Mkoa wa Njombe na mingineyo nchini haipo sababu ya kuwa na tatizo la uhaba wa nyumba za askari kwani kuna fursa ya kutosha ya kufyatua tofali za kuchoma  kwa kuwatumia wafungwa ili kumaliza tatizo hili nchini”. Amesisitiza Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amewataka mafisa na askari wote kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo.

Awali, akisoma taarifa ya Gereza la Wilaya Njombe, Mkuu wa Gereza hilo, SP. Charls Mihinga amesema kuwa  tayari wameanzisha mradi wa ufyatuaji wa tofali za kuchoma katika kambi ya mdandu ili kumaliza tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi wa gereza hilo.

“Katika msimu huu tumeweza kufyatua tofali kubwa zipatazo 30,000 ambazo tayari zimeshachomwa, tofali hizi zitatumika katika ujenzi wa nyumba za askari pamoja na ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Magereza Mkoani Njombe”. Alisema SP. Mihinga.

Pia, ameongeza kuwa  malengo ya baadaye ni kuifanya kambi hiyo ya Gereza Njombe kuwa na taswira ya uzalishaji wa matofali kwa wingi kwa ajili ya kufanya biashara na hivyo kuongeza maduhuri serikalini.

Jeshi la Magereza linakabiliwa na uhaba wa nyumba za kuishi za Maafisa na askari hapa nchini, mkakati uliopo hivi sasa chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali wa Magereza ni kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatulika kwa kutumia njia ya ubunifu pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jeshi hilo.