Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro  Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka akitoa taarifa ya utendaji katika mkoa wake kwa Kaimu Kamishna Magereza Dr. Juma Malewa (hayupo pichani) mwishoni mwa juma hili alipofanya ziara ya kiutendaji katika baadhi ya Magereza mkoani humo.

 
Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa katika hali ya kuamsha hari na morali ya kufanya kazi kwa watendaji wa Jeshi la Magereza amefanya ziara ya kikazi katika baadhi ya Magereza ya Mkoa wa Morogoro na Pwani mwishoni juma hili.

Ziara hiyo imejumuisha Magereza ya Mbigiri, Wami Kuu, Wami Vijna, Mahabusu, Kihonda, Kingolwira Complex yote ya mkoa wa Morogoro na Shule ya Sekondari Bwawani na gereza Ubena vya mkoani Pwani.

Kutoka kwa Kaimu Jenerali maafisa na askari aliwapata taarifa fupi ya Uwekezaji wa Ubia katika kiwanda cha sukari cha gereza Mbigiri Mkoani Morogoro kati ya Jeshi la Magereza na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF. Alisema uwekezaji huu ni kwa faida ya Jeshi kama Taasisi hivyo ni vizuri kila askari akalifahamu hilo.

Katika ziara hiyo pia alipata wasaa wa kufanya vikao na watendaji ambapo maafsa, askari na watumishi raia walipata fursa ya kuuliza maswali moja kwa moja kutoka kwa Mtendaji mkuu wa Jeshi la Magereza ambapo baadhi ya mambo yalipatiwa majibu ya papo hapo na mengine kupewa ahadi ya kutatuliwa katika siku za usoni hasa yenye uhusiano na masuala ya kibajeti.

Miongoni mwa masuala yaliyoonekana kuwa ni tatizo sugu ni pamoja na huduma za maji, usafiri, matibabu kwa wafungwa na mahabusu, sare za askari, posho mbalimbali kulingana na stahiki ya kila askari  na mambo mengine madogo madogo ambayo yote kimsingi yanagusia suala la fedha.

Katika vikao hivyo Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Juma Malewa alitolea maelekezo baadhi ya mambo yaliyohitaji kauli ya Makao Makuu ya Jeshi lakini pia aliwahakikishia kuwa ofisi yake itaendelea kushughulikia kero zote na kusaidia kwa haraka pale inapohitaji kwa kutegemeana na hali ya fedha kwa wakati huo.

Kaimu Kamishna Jenerali aliwaasa maafisa askari kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kijamii hasa kwa kuzingatia viapo vya utumishi wao.
“Ninyi ni askari wenye viapo vya utii wa mamlaka zilizopo, jiepusheni na mijadala ya mitandaoni kwani mingine iko kinyume na maadili ya kazi zetu. Ukipokea ujumbe usiofaa futa kabisa badala ya kuusambaza” alisisitiza Dr. Malewa

Aidha Dr. Malewa aliwataarifu watumishi hao adhma yake kuu ya kuona Jeshi linakuwa na hospitali kubwa nayakisasa ili kuondoa kero na aibu inayowapata askari na familia zao wanapokuja kutibiwa Jijini Dar es salaam.

Ni dhamira yangu kuona tunaanzisha ujenzi wa hospitali hivi karibuni ili kuondoka na adha ambayo wote mnaifahamu, na hospitali hii tutaijenga kwa kutumia vyanzo mbali mbali ikiwemo na sisi kama askari kujitolea. Naomba mtuunge mkono mara wazo hili litakapoletwa kwenu” alisisitiza Kaimu Jenerali.

Mwisho aliwataka maafisa na askari kudumisha nidhamu kazini ikiwa ndiyo msingi mkuu wa mafanikio hasa katika kazi za majeshi.

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com