Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(katikati) katika Jukwaa akipokea Salaam kutoka kwa Gwaride la Wahitimu wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza(hawapo pichani) katika hafla ya kufunga Mafunzo hayo leo Julai 9, 2016 Chuo cha Magereza, Kiwira Mbeya. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP- John Casmir Minja.

 

Na; Lucas Mboje, Rungwe

JUMLA ya Wahitimu 1364 wa Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza wamehitimu kuwa Askari kamili wa Jeshi hilo ambapo kati yao wanaume ni 977 na wanawake 377, Mafunzo hayo yamefungwa rasmi Julai 9, 2016 katika Chuo cha Magereza Kiwira, Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.

Akizungumza katika sherehe za kufunga Mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amesema Askari wote wa Jeshi la Magereza nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kila wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Aidha, Meja Jenerali Rwegasira amewataka  Askari wahitimu wakazingatie elimu waliyopewa wakati wa mafunzo ili kuwezesha kuongezeka kwa ufanisi katika majukumu ya Jeshi la Magereza.

Sambamba na hilo, amewaasa kudumisha nidhamu mahala pa kazi kwani nidhamu ndiyo msingi wa kufanikisha utendaji kazi mahala pa kazi hususani katika Taasisi za Kijeshi.

"Hivyo ili kudumisha utendaji wenu wa kazi, mnapaswa kuzingatia nidhamu katika utekelezaji wenu wa majukumu yenu kulingana na maelekezo mtakayokuwa mnapewa". Alisisitiza Meja Jenerali Rwegasira.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja amesema kuwa changamoto nyingi ambazo kwa kiasi fulani zimeathili utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo ni pamoja na ufinyu wa bajeti, makazi duni ya maafisa na askari, uhaba wa vitendea kazi na uchakavu wa vyombo vya usafiri.

Kamishna Jenerali Minja ameongeza kuwa tayari Jeshi hilo limechukua hatua mbalimbali za kufanya maboresho kwa lengo la kufanya Jeshi la Magereza kuwa la kisasa katika kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi unaotarajiwa.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com