Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amelitaka Jeshi la Polisi kuangalia aina ya makosa ya watuhumiwa ambayo yana dhaminika ili kupunguza mlundikano wa mahabusu Magerezani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua miradi ya maendeleo ya Jeshi la Magereza na baadaye kuzungumza na Maafisa na Askari wa Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma, leo, Simbachawene alisema Jeshi hilo linakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya mahabusu ukilinganisha na wafungwa waliopo magerezani.

“Mlundikano wa mahabusu magerezani ni changamoto kubwa, lakini inapaswa kuangaliwa kwa upana zaidi, hasa kwa Jeshi la Polisi kuangalia makosa yanayodhaminika ili wasizalishe mahabusu kwasababu zisizo za msingi,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, kwa kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano magerezani sambamba na kuipunguzia Serikali gharama ya kuwahudumia wafungwa na mahabusu.

“Tunajaza magereza yetu kwa kuzalisha mahabusu kwa makosa ambayo mengine hayastahili kuwaleta magerezani kama vile ugomvi wa kifamilia na makosa mengine madogo madogo ambayo yanadhaminika,” alisisitiza Simbachawene.

Aidha, akitoa taarifa ya Jeshi hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Suleiman Mzee alisema kwasasa kuna wafungwa 14,502 na mahabusu 17,396 katika magereza yote nchini.

“Tutajitahidi kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika jukwaa letu la haki jinai ili kuangalia namna bora ya kutatua tatizo au changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani,” alisema Kamishna Jenerali Mzee.

Kamshina Jenerali Mzee alimshukuru Waziri Simbachawene kwa kufanya ziara Makao Makuu ya Magereza na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo mbalimbali aliyoyatoa kwa Jeshi hilo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. kwa habari picha Zaidi Bofya hapa