Na Lucas Mboje, Jeshi la Magereza

BODI ya Taifa ya Parole ya Awamu ya Tano imeelezea mafanikio mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu ambapo Bodi hiyo imewezesha kuachiliwa jumla ya wafungwa 648 katika mpango huo wa Parole na hadi sasa hakuna mfungwa yeyote aliyevunja masharti ya Parole na kurudishwa gerezani.

Hayo yamesemwa mapema leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Agustino Mrema katika Kikao cha 41 cha Bodi hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Maafisa Magereza Ukonga, jijini Dare es Salaam.

 “Jumla ya wafungwa 666 wamejadiliwa na Bodi ya Taifa ya Parole katika vikao vyake saba vilivyofanyika na kupendekeza kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo wafungwa 648 wamenufaika na mpango huo na wafungwa 18 hawakupendekezwa kutokana na sababu mbalimbali”. Amesema Mhe. Mrema.

Amesema kuwa katika utendaji wa Bodi yake kwa miaka mitatu umechangia kuimarika kwa hali ya utulivu na usalama ndani ya magereza kwa wafungwa kwani wamekuwa na matumaini makubwa ya kuingizwa kwenye mpango huo sanjari na kupokea programu za urekebishaji katika magereza mbalimbali nchini.

Mafanikio mengine ni kuwa Wafungwa walioachiliwa katika mpango huo katika kipindi hiki wameshiriki na wanaendelea kushiriki vyema katika shughuli za maendeleo katika jamii zao ikiwemo kuziangalia na kuzihudumia familia zao; hivyo kuipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia wafungwa hao kama wangekuwepo magerezani. 

Aidha, Mhe. Mrema amezungumzia changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Bodi hiyo ikiwemo ufinyu wa bajeti katika kufanikisha shughuli za Bodi. Changomoto zingine ni katika maeneo ya kiutawala, kisheria ambazo hata hivyo amesema hatua mbalimbali za utatuzi zinaendelea kufanyiwa kazi na mamlaka husika.

“Bodi hii ya tano imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka mitatu, licha ya changamoto hizo nilizozitaja, kipekee nitoe shukrani za dhati kwa wajumbe wa Bodi kwa ushirikiano wao kwangu. Pia natoa shukrani za kipekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi hii katika kutekeleza matakwa ya Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400”. Amesema Mhe. Mrema.

Bodi ya Taifa ya Parole ya Awamu ya Tano ilizinduliwa na kuanza kufanya kazi zake Machi 21, 2019 na inatarajia kumaliza muda wake wa kuwa madarakani kwa miaka mitatu ifikapo Julai 16, 2019.