Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike akizungumza na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza katika Baraza la kufunga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019 leo Desemba 31, 2018 Makao Makuu ya Jeshi la Magereza. (Picha na Jeshi la Magereza)

 

Na ASP Deodatus Kazinja
Katika kufunga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019  Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ameelezea matarajio ya Jeshi hilo kwa mwaka 2019 kuwa ni pamoja  kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia katika kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu.

Matarajio mengine ni pamoja na  kumimarisha hali ya ulinzi na usalama magerezani ikiwa ni pamoja na kusimika mifumo ya kiusalama, kujenga kiwanda cha seremala mkoani Dodoma ili kuongeza na kuimarisha  utengenezaji wa samani, kujenga nyumba 100 mkoani Dodoma kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Makao makuu mkoani humo.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike ameongeza kuwa matarajio ya mwaka ujao ni  Kuanzisha ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Makao Makuu mkoani Dodoma, kuendelea kuhimiza ujenzi wa nyumba kwa njia ya kujitolea ili kupunguza uhaba wa nyumba za watumishi wa jeshi hilo,

Pia amesema atahakikisha Shirika la Magereza (Magereza Corporation Sole) linapata Bodi ili kujiimarisha katika kufanya shughuli za kibiashara. Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza litashirikiana na Idara ya mahakama katika kukamilisha maandalizi ya uendeshaji wa mashauri kwa mfumo wa kielektroniki wa ‘video conference’ ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wafungwa na mahabusu kwa wakati.

Kamishna Jenerali Kasike amehitimisha Salaam za Mwaka Mpya kwa kusisitiza suala la ufanyaji kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Jeshi hilo na amewataka askari kubadili mtazamo wa kiutendaji na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. “Kila mmoja atimize wajibu wake kikamilifu kwa kutumia uweledi, ubunifu na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele”.

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com