Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike akisalimiana na maafisa wa gereza Mpwapwa mkoani Dodoma alipowasili kituoni hapo kwa ziara ya kikazi Agosti 14,2018

(Picha na Jeshi la Magereza.)

 

Na Deodatus Kazinja

Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza nchini wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kujinufaisha na mali za Jeshi hilo kinyume na utaratibu.

Hayo yalisemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo Phaustine Kasike wakati akizungumza na maafisa na askari wa gereza Mpwapwa na Kongwa kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kikazi katika vituo hivyo Agosti 14 mwaka huu.

Kamishna Kasike alisema si jambo la kificho kukuta shamba, mifugo na mali nyinginezo za gereza zinamilikiwa na kuendeshwa na mkuu wa gereza kama mali yake binafsi.
Mkuu huyo wa magereza nchini akionesha kukasirika alisema siyo siri kukuta shamba la mkuu wa gereza au mkuu wa magereza wa mkoa likiwa limestawi huku shamba la serikali limesinyaa kabisa kwa visingizio vya hali ya hewa wakati vyote viko sehemu moja na vinatumia nguvu kazi ya wafungwa na raslimali nyinginezo hizo hizo za serikali.

“Nawataka maafisa na askari ndani ya Jeshi la Magereza kutambua kuwa tabia za namna hii ndizo zimesababisha Jeshi letu kutosonga mbele. Tunatazamwa kama watu tulioshindwa kutimiza wajibu wetu kwa tabia zetu za udokozi, wizi na ubinafsi na tunaoweza kurekebisha hali hii ni sisi wenyewe” alisema Kamishna Kasike.

Akitolea mfano wa mifugo kama ng’ombe na mbuzi Jenerali Kasike alisema ni jambo la kawaida kukuta kituo kiko na idadi hiyo hiyo ya mifugo kwa miaka kadhaa bila kuongezeka mfugo hata mmoja na ikiwa kuna mabadiliko ni ya kupungua tena kwasababu ambazo hazina mashiko.

“ Binafsi nakataa. Mwaka mzima ng’ombe au mbuzi wasiongezeke haiwezekani. Ni ubadhilifu tu. Nataka kila mmoja atambue kuwa zama hizo zimekwisha na niseme ni ama unabadilika au tunashughulikiana ” Alisema Kamishna Jenerali Kasike.

Na kuongeza “wakati serikali inatutaka tuzalishe chakula cha kujitosheleza kwa wafungwa na ziada tuuze ili tuingize maduhuli serikalini ni lazima kubadilika kabisa kiutendaji ili kufikia lengo hilo.”

Naye mmoja wa askari wa gereza Mpwapwa akichangia katika kikao hicho alisema wao kama watendaji wa ngazi za chini wako tayari kumuunga mkono Kamishna Jenerali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika kuifanya magereza mpya endapo na viongozi wao katika vituo watakuwa wepesi wa kuwa wabunifu na kupokea ushauri kutoka kwao.

Akitolea mfano wa ng’ombe wanaokufa wakati wa kiangazi katika baadhi ya maeneo askari huyo alisema ni jambo la kushangaza kuona ng’ombe wanakufa kwa kukosa maji wakati ng’ombe wasiozidi kumi wakiuzwa wanatosha kugharimia huduma za kuchimba kisima ili kunusuru walio wengi.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali Kasike alikubaliana na askari huyo akisema wakati mwingine tumefika hapa kutokana na baadhi ya viongozi kushindwa kuwa wabunifu na kutotaka kupokea ushauri kutoka kwa walio chini yao.

“ Mimi ni muumini wa uongozi shirikishi. Natoa wito kwa viongozi wote katika Jeshi letu kushirikisha wataalam bila kujali vyeo vyao. Pokeeni mawazo na ushauri. Cheo ni ngazi tu lakini mawazo ya mtu yanaweza kuwa ya msingi sana.Alihitimisha Kamishna Kasike.

Kamishna Jenerali Kasike amehitimisha ziara ya kikazi mkoani Dodoma iliyomfikisha katika ofisi mpya ya Makao Makuu ya Magereza mkoani humo, gereza Isanga, Msalato, Mpwapwa na Kongwa.

Akiwa mkoani humo amezungumza na maafisa na askari ambapo ujumbe wake mkuu kubadilika kabisa kwa namna tunavyofanya kazi. Aidha, ametembelea miradi mbalimbali ikwemo ufyatuaji matofali, ujenzi wa nyumba za kuishi za maafisa na askari kwa njia ya kujitolea, mradi wa upigaji kokoto wa Msalato, shamba la zabibu-Isanga na shamba la korosho la gereza Mpwapwa.

 

Kwa habai picha zaudi tembelea www.magereza.blogspot.com