Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike(miwani) akiangalia mabwawa ya kufugia samaki katika Gereza Kwamngumi alipotembelea leo Agosti 4, 2018, Wilayani Korogwe(kushoto) ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga.

(Picha na Jeshi la Magereza)


Na Lucas Mboje, Magereza;

MRADI wa ufugaji wa samaki wa Gereza Kwamngumi wenye mabwawa 30 utawekewa mkakati wa kuwezesha uzalishaji wa samaki wa kutosha ili kutoa faida kubwa kwa Jeshi la Magereza pamoja na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo Agosti 4, 2018 na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya kwenye mradi wa ufugaji samaki ya Gereza Kwamngumi, lililopo Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.

Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa ziara yake ililenga kujionea maendeleo ya mradi wa uzalishaji wa samaki kwenye Gereza hilo ili kuweza kuuboresha zaidi.

“Nimeshuhudia eneo hili lina fursa nzuri katika ufugaji wa samaki wa aina mbalimbali kwani mabwawa yapo yakutosha na chanzo cha maji ya uhakika nitahakikisha mradi huu unasimamiwa vizuri ili ulete tija”. Alisema Jenerali Kasike.

Kabla ya kutembelea eneo la mradi wa mabwawa ya samaki, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini amepokea taarifa ya Mkoa ya utendaji kazi wa Jeshi hilo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga pamoja na kuzungumza na Maofisa na askari wa Gereza Korogwe.

Akiwasilisha taarifa yake mbele ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga amesema kuwa magereza ya mkoa wa tanga yana fursa ya ardhi yakutosha na yenye rutuba inayofaa kwa kilimo hivyo watajitahidi kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa na mahabusu.

“Afande Jenerali nikuhakikishie tu kuwa maagizo yaliyotolewa na Rais Dkt. Magufuli kuhusu wafungwa kujitosheleza kwa chakula, sisi mkoa wa tanga tupo tayari kutekeleza jukumu hilo”. Alisema Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa.

Mradi wa uzalishaji samaki katika Gereza Kwamugumi, Wilayani Korogwe ni mojawapo ya miradi mbalimbali ya uzalishaji mali iliyoanzishwa na Jeshi hilo ambapo ikisimamiwa kimkakati wa kibiashara inaweza kuipunguzia serikali gharama za kuhudumia Jeshi la Magereza na pia kuongeza pato la kodi kwa Taifa.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com