Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akisalimiana na Mkuu wa Kiwanda cha Viatu Gereza Kuu Karanga, Moshi, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Hezron Nganoga alipotembelea kiwanda hicho kukagua maboresho ya ufungaji wa mashine mpya za kutengenezea viatu vya aina mbalimbali ikiwemo buti zinazotumiwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama hapa nchini leo Agosti 1, 2018.  Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.

(Picha na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Makao Makuu ya  Jeshi la Magereza).

 

Na Mwandishi wetu; Magereza

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ameridhishwa na maboresho yanayoendelea ya usimikaji wa mashine mpya katika Kiwanda cha zamani cha viatu cha Gereza Kuu Karanga Moshi.

Akizungumza na wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro leo Agosti 1, 2018 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini mara baada ya kutembelea Kiwanda hicho cha ubia kati ya uliokuwa mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF na Jeshi la Magereza amesema kiwanda hicho kitaongeza uzalishaji wa viatu hivyo kukidhi mahitaji kwa wateja wake tofauti na kipindi cha zamani.

“Kiwanda chetu cha Karanga baada ya maboresho haya ndugu waandishi kama mlivyoshuhudia kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jozi 400 kwa siku kutoka jozi 150 zilizokuwazikizalishwa hapo zamani”. Alisema Kamishna Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike ametoa wito kwa wananchi wote kutumia bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho kwani zinaubora wa hali ya juu na waondokane na mtizamo wa kupenda zaidi bidhaa za kutoka nje ya nchi bali wawe wazalendo kwa kutumia bidhaa za ndani.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Viwanda vya ngozi – Gereza Kuu Karanga, Bw. Masoud Omary amesema kuwa kiwanda hicho kwa sasa kipo kwenye hatua za mwisho za kukamilika ufungaji wa mitambo mbalimbali ya kukata ngozi, ushonaji, uwekaji soli za viatu pamoja na mashine nyinginezo ili kuongeza ubora wa viatu.

Ameongeza kuwa hadi sasa mitambo hiyo imegharimu kiasi cha shillingi bilioni 2.7 na maboresho mengine ambayo yamefanika ni maboresho ya mfumo wa umeme wa kiwanda hicho pamoja na jengo la kiwanda.

Kiwanda cha viatu cha Gereza Kuu Karanga, Moshi kilizinduliwa rasmi Juni 3, 1977 na Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Kambrage Nyerere.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com