UJUMBE KUTOKA KWA KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI
Jeshi la Magereza lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na lilianzishwa rasmi kama idara inayojitegemea mnamo tarehe 25 Agosti, 1931. Kabla ya kuanzishwa kwake utekelezaji wa majukumu yake ulikuwa unafanyika kwa pamoja na Jeshi la Polisi. Lengo kuu lilikuwa kuwalinda wafungwa wasitoroke na kuwafanyisha kazi ngumu wafungwa waliohukumiwa.

Pamoja na Jeshi hili kujitenga, utendaji haukubadilika sana hasa katika kuwahudumia wafungwa na mahabusu kwani lengo kuu lilibaki lilelile la kuwalinda wafungwa wasitoroke, na kuwafanyisha kazi ngumu.

Baada ya uhuru tarehe 9 Desemba, 1961 utendaji wa kazi ulibadilika kwa kuingiza fikra mpya katika uendeshaji wa magereza ambapo pamoja na mambo mengine masuala ya haki za binadamu yalizingatiwa katika kuwahudumia wafungwa na mahabusu na dhana ya urekebishaji ilianza kushika kasi.

Mabadiliko haya yalipewa nguvu za kisheria kwa kutungwa kwa sheria ya Magereza ya mwaka 1967, iliyowezesha kutungwa kwa Kanuni, Miongozo na taratibu mbalimbali katika uendeshaji wa Jeshi la Magereza. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine zilizingatia mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya haki za binadamu katika utunzaji na uhudumiaji wa wafungwa.

Jeshi la Magereza ni mojawapo ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Majukumu yake ni kuchangia katika kuleta, kuendeleza na kudumisha usalama wa jamii nchini kwa kufanya yafuatayo:-
i) Kuwahifadhi wafungwa wa aina zote wanaowekwa gerezani kwa mujibu wa sheria;
ii) Kuandaa na kutekeleza programu za urekebishaji wa wahalifu kwa kuwafundisha shughuli mbalimbali za uzalishaji na ujuzi kwa njia ya vitendo na ushauri;
iii) Kuendesha shughuli na huduma kwa wafungwa kwa mujibu wa Sheria;
iv) Kuchangia katika ushauri kuhusu uzuiaji na udhibiti wa uhalifu na urekebishaji.

Pamoja na majukumu hayo Jeshi la Magereza vilevile hutoa wataalam wake wenye fani mbalimbali ili kusaidia kuimarisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani (United Nations Peacekeeping Mission – UNPM).
Tangu Jeshi hili lianzishwe, limetekeleza majukumu yake ya msingi kwa mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri baina yake, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla.

Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na uzalishaji wa mazao mbalimbali yanayoliingizia Taifa kipato cha kuridhisha na hivyo kuchangia gharama za matunzo ya Wafungwa wenyewe, vituo vya Magereza nchini pia vimeendelea kutumika kama maeneo ya uelemishaji wa wananchi(Extension units) kuhusu mbinu za kisasa za kilimo, ufugaji, uzalishaji wa mbegu bora za kilimo na bidhaa za viwanda vidogovidogo.

Aidha, Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake limefikia makubaliano na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ambao wamevutiwa na shughuli zetu kwa lengo la kuingia ubia ili kukuza mitaji na kubadilishana ujuzi katika miradi mbalimbali ikiwemo ya Madini na Kilimo.

Pia, Jeshi la Magereza tayari limeandaa Rasimu ya Mpango wa Maboresho na Sera ya Taifa ya Magereza na hivi sasa mchakato wa maandalizi ya mwisho ya mpango huo unaendelea vizuri ili kuuwasilisha serikalini. Kukamilika kwa mpango huo wa Maboresho kutalifanya Jeshi la Magereza kuwa bora na la kisasa linalotoa huduma zinazolingana na matakwa ya Kanuni za Sayansi ya Urekebishaji katika Uendeshaji wa Magereza.

Pamoja na changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi letu, namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama pamoja na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zake mbalimbali za kuendelea kulijengea uwezo Jeshi letu kwa kulipatia rasilimali fedha na watu, vitendea kazi katika kutekeleza majukumu yetu ipasavyo.

Aidha, natoa pongezi za dhati kwa Maofisa, Askari Magereza na Watumishi wote wa ngazi na fani mbalimbali kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii, utii, uhodari, nidhamu, uadilifu na weledi, hivyo kutimiza matakwa ya Dhima na Dira ya Jeshi letu la Magereza.

Shukrani za dhati nazielekeza pia kwa jamii na wadau mbalimbali kwa kushirikiana vyema na Jeshi la Magereza katika kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Ushirikiano huo ni muhimu uendelee kudumishwa wakati wote.

Jeshi la Magereza litaendelea kutekeleza wajibu wake na kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama pamoja na Umma wa Watanzania kwa ujumla katika kudumisha amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi hapa nchini.

Aksanteni kwa Ushirikiano.

.