Na Lucas Mboje, Dar es Salaam;

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira(pichani) amewataka Maafisa na Askari wote wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi kudumisha nidhamu wanapokuwa wakitekeleza majukumu ya kazi za kila siku.

Meja Jenerali Rwegasira ameyasema hayo leo katika hafla ya ufungaji Mafunzo ya Uongozi wa ngazi za juu kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam.

"Katika muda mfupi niliofanya kazi katika Wizara hii nimeambiwa kuna watumishi wanakataa kwenda kwenye vituo vipya kwasababu ya kutopatiwa fedha za uhamisho, huo ni utovu wa nidhamu," Alisema Jenerali Rwegasira.

Alisisitiza Mtumishi anapopatiwa uhamisho ndani ya Jeshi jambo la kwanza ni Utii kwanza wa Utekelezaji wa Amri hiyo na siyo sababu au madai mengine ambayo ni kinyume na Utendaji wa Taasisi za Kijeshi.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, CGP. John Casmir Minja alisema Jeshi hilo limeitikia wito wa kubana matumizi kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph Pombe Magufuli ndiyo maana katika hafla hiyo imehusisha Maafisa wachache wa Gwaride ili kupunguza gharama zisizo za Msingi.

"Katika Sherehe za kufunga Mafunzo ya Uongozi kwa mwaka huu Gwaride limepunguzwa kwa kujumuisha Maafisa na Askari wachache zaidi na pia hata Wageni Waalikwa utaona wamekua ni wachache sana ili kuitikia wito wa Rais wa Awamu ya tano kama anavyosisitiza kupunguza matumizi yasiyoyalazima" Alisema Kamishna Jenerali John Casmir Minja.

Aidha, alisema Chuo hicho kina changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu baada ya kupewa hadhi ya kuwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji na kwamba anaamini Serikali ya awamu ya tano itazifanyia kazi changamoto hizo.

Hata hivyo Kamishna Jenerali Minja aliwapongeza wahitimu hao kwa kuchangia Tsh. Milioni 2.4 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya chuo hicho kwa ridhaa yao ambapo walichangishana fedha hiyo ili kuboresha hali ya chuo hicho.

Jumla ya Wahitimu 98 wa Mafunzo ya Uongozi ngazi za Juu wamehitimu Kozi hiyo na kutunukiwa cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Magereza ambapo Idadi hiyo inajumuisha Wahitimu 93 kutoka Tanzania Bara ikiwa Wanaume ni 83 na Wanawake 10 pamoja na Wahitimu 05 kutoka Vyuo vya Mafunzo Zanzibar ambao ni Wanaume 04 na Mwanamke 01.