Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuapisha Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu kuwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Magereza katika hafla fupi iliyofanyika Julai 31, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uapisho huo Rais Samia alimvisha cheo kipya cha Kamishna Jenerali ambacho uteuzi wake ulianza rasmi Julai 28, 2024. Aidha, kabla ya kuteuliwa kushika nafsi hiyo, Katungu alikuwa akihudumu nafasi ya Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Magereza.
Kamishna Jenerali Katungu (CGP) amechukua nafasi hiyo kufuatia aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo Kamishna Jenerali Alhaji Mzee Ramadhani Nyamka kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria.
Je, CGP Jeremiah Yoram Katungu ni nani?
CGP. Jeremiah Yoram Katungu alizaliwa mwaka 1970 katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida na alipata Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Makasuku, Manyoni mwaka 1978-1984 na Elimu ya Sekondari (O-Level) katika Shule ya Sekondari Mwenge, Singida mwaka 1985-1988.
Mwaka 1989-1991 alijiunga na elimu ya juu ya sekondari (Advanced level) katika Shule ya Sekondari Galanos mkoani Tanga ambapo alihitimu kidato cha sita, na mwaka 1993-1996 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo alihitimu Shahada ya Kwanza ya Sanaa (Bachelor Degree of Arts with Honors). Aidha, Agosti 30, 2015 alijiunga na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na kuhitimu Julai 23, 2016.
Kujiunga na Jeshi la Magereza
CGP. Jeremia Yoram Katungu alijiunga na Jeshi la Magereza Julai 8, 1998 ambapo alihuhudhuria mafunzo ya awali katika Chuo cha Maafisa wa Magereza Kiwira, Mbeya na kuhitimu mafunzo hayo Desemba 8,1998 na mara baada ya kuhitimu alipangiwa mkoa wa Dar es Salaam, kituo cha kazi Gereza Segerea ambapo alifanya kazi mpaka mwaka 2007 alipohamishiwa Makao Makuu ya Magereza kituo anachofanya kazi mpaka sasa.
Kupandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali
Katika utumishi wake ndani ya Jeshi la Magereza alipandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo kuwa Wada wa Magereza (WDR) 1998, Mkaguzi Msaidizi wa Magereza (A/Insp) 1998 -2003, Mkaguzi wa Magereza (Insp) 2003-2006, Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) 2006-2010, Mrakibu wa Magereza (SP) 2010-2012, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) 2012-2015, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) 2015-2017, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) 2017-2018, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) 2018- 2024, Kamishna wa Magereza (CP) Juni, 2024 na Julai 28, 2024 akateuliwa kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP).
Nishani alizowahi kutunukiwa
Mbali na kupandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali, CGP. Katungu katika utumishi wake ametunukiwa Nishani mbalimbali zikiwemo Nishani ya Utumishi Uliotukuka, Utumishi wa Muda Mrefu kazini na Nishani ya Miaka 60 ya Muungano.
CGP. Katungu anakuwa Mkuu wa Jeshi la Magereza wa 16 tangu kupatikana kwa uhuru mwaka 1961. Watangulizi wake ni Patrick Manley (1955-1962), Obadia Rugimbana (1962-1967), Ramadhani Nyamka (1967-1978), Ambindwile Mwaijande (1978-1978) ambao wote ni marehemu.
Wakuu wastaafu wa Jeshi la Magereza wengine ni Gabriel Geneya (1979-1983) sasa ni marehemu, Simon Mwanguku (1983-1992) sasa ni marehemu, Jumanne Mangara (1992-1996), Onel Malisa (1996-2002) sasa ni marehemu, Nicas Banzi (2002-2007), Agustino Nanyaro (2007-2012), John Minja (2012-2016), Dkt, Juma Malewa (2016-2018), Phaustine Kasike (2018-2020), Meja Jenerali Suleman Mungiya Mzee (2020-2022) na Alhaji Mzee Ramadhani Nyamka (2022-2024).