Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt. Maduhu Kazi, akisaini kitabu cha wageni ndani ya ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee, mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato Jijini Dodoma, kwa ziara ya kikazi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt. Maduhu Kazi, leo Mei 25, 2022 ametembelea Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato Jijini Dodoma, na kupokelewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, na Maafisa waandamizi wa Magereza, lengo likiwa ni kujitambulisha kwa Jeshi la Magereza, kuzungumza na Maafisa na Askari na kutembelea miradi mbalimbali inayo tekelezwa na Jeshi la Magereza Makao Makuu.

Akizungumza na Maafisa na Askari, Mhe. Maduhu amesema, anaupongeza uongozi wa Jeshi la Magereza chini ya CGP.Mzee, na watumishi wote wa Jeshi Nchi nzima, kwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanyika katika kuleta maendeleo ndani Jeshi, huku akiahidi kushirikiana na viongozi ndani ya Jeshi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazo wakabili Maafisa na Askari na Jeshi kwaujumla.

Awali kabla ya kumkaribisha Mhe.Maduhu kuzungumza na Maafisa na Askari, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee alitoa maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza Nchi nzima, hivyo kumpa fursa Naibu Katibu Mkuu Mhe. Dkt.Maduhu ya kuona kwa picha shughuli na miradi inayoendelea kutekelezwa katika vituo vya Magereza.

Ziara hiyo ya Mhe.Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Maduhu Kazi, ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kushika nafasi hiyo ya uongozi, imehitimishwa kwa kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Kiwanda cha Samani Magereza Msalato, Nyumba za Makazi ya Maafisa na Askari na Kituo cha kibiashara Isanga (ISANGA PRISONS BUSSINESS CENTRE).