Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan, akimvisha Nishani ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, Desemba 09, 2021  Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kiwanda cha Samani cha Jeshi la Magereza kilichopo Msalato Jijini Dodoma

Baadhi ya nyumba za kisasa za makazi ya Maafisa na Askari, zilizopo Msalato Jijini Dodoma.

Kituo cha Biashara Gereza Isanga (ISANGA PRISON BUSSINESS CENTRE)

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Jumanne Sagini (Mb), (Wa nne kutoka kulia), mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi katika ghala la kuhifadhia mazao Gereza Idete mkoani Morogoro, Januari 29, 2022.

FUNGU 29: JESHI LA MAGEREZA

Utangulizi:

 Jeshi la Magereza ni mojawapo ya Idara zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambalo linaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 [Sura ya 58 RE.2002] pamoja na kanuni zake.

Dira na dhima ya Jeshi la Magereza

Katika miaka ya 1990 Jeshi la Magereza lilianzisha dira na dhima yake kulingana na mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza.

Dira ya Jeshi la Magereza ni kuwa Jeshi la kurekebisha wahalifu lenye utaalamu wa hali ya juu linaloendeshwa na kanuni na viwango vilivyowekwa Kitaifa na Kimataifa.

Dhima ya Jeshi la Magereza ni kutekeleza wajibu ipasavyo katika kuimarisha ulinzi wa jamii kupitia usimamizi wa kifungo na kuwasimamia wahalifu, huduma za mahabusu, programu na huduma zinazoshughulikia mahitaji ya urekebishaji wa wahalifu na ushauri wa kisera kuhusu uzuiaji wa uhalifu na ushughulikiaji wa wahalifu.

Majukumu na malengo ya Jeshi la Magereza

Majukumu ya Jeshi la Magereza ni kuchangia katika kuleta, kuendeleza na kudumisha usalama wa jamii nchini kwa kufanya yafuatayo:-

Kuwahifadhi wafungwa wa aina zote wanaowekwa chini ya ulinzi halali kisheria ndani ya magereza.

Kuandaa na kutekeleza programu za urekebishaji wa wahalifu na kuwafundisha shughuli za uzalishaji na ujuzi mbalimbali kwa njia ya vitendo na ushauri.

Kuendesha shughuli na huduma za watuhumiwa (Mahabusu) kwa mujibu wa sheria.

Kuchangia katika ushauri kuhusu uzuiaji na udhibiti wa uhalifu na urekebishaji wahalifu.

Kwa kuwahifadhi wafungwa katika mazingira ambayo ni salama, Jeshi la Magereza linalenga kuilinda jamii dhidi ya wahalifu hao hivyo kuiwezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji kwaajili ya kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, kupitia utoaji wa programu za urekebishaji na ufundishaji wa shughuli za uzalishaji na ulinzi, Jeshi la Magereza linalenga kuwawezesha wahalifu kuachana na mienendo ya kihalifu Magerezani na watakaporejea kwenye jamii baada ya vifungo vyao waishi maisha yanayozingatia sheria za nchi.

Mafanikio ya Jeshi la Magereza katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita

Mnamo tarehe 19 Machi, 2021 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan aliapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais Samia alichukua nafasi hiyo kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam na baadaye kuzikwa Machi 26, 2021 nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Kimsingi, huwezi kuyataja mafanikio yaliyofikiwa na watangulizi wake bila kumtaja Mh. Samia Suluhu Hassan kwani kwa nyakati tofauti amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika awamu hizo hivyo kushiriki kwa namna moja au nyingine kuleta mafanikio ya Serikali hizo.

Lakini kipekee kabisa ni kipindi hiki ambacho yeye mwenyewe Mh, Rais Samia Suluhu Hassan ameshika hatamu za uongozi, ingawa bado ni kipindi kifupi lakini huwezi kuacha kuyaeleza mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa na Serikali yake katika kila nyanja mpaka hivi sasa anapoelekea kutimiza mwaka mmoja.

Jeshi la Magereza kama chombo kilichokabidhiwa dhamana ya urekebishaji wa tabia za wahalifu ni moja ya Taasisi ambayo inajivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita iliyo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 Rasilimali watu:

 • Ajira

Jeshi la Magereza likiwa moja ya taasisi ya serikali lilipewa nafasi 700 za ajira kwa vijana wenye sifa mbalimbali zilizoainishwa ambao wapo katika mafunzo ya awali ya kijeshi katika Chuo Cha Magereza Kiwira- Mbeya. Kuajiriwa kwa askari hao kutapunguza kwa kiasi tatizo la upungufu wa watumishi ambao umetokana na kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa kazi, kufariki na utoro kazini.

 • Kupandishwa vyeo

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, jumla ya maafisa na askari 8,736 wamepandishwa vyeo mbalimbali kwa wakati mmoja. Kati ya idadi hiyo, maafisa na askari waliopandishwa vyeo kwa utaratibu wa kawaida wa bila kuhudhuria mafunzo, walikuwa kama ifuatavyo:-

Kamishna Wasaidizi wa Magereza  (ACP)            26

Warakibu Waandamizi wa Magereza (SSP)         61

Warakibu wa Magereza  (SP)                    ­­­           174

Wakaguzi wa Magereza  (INSP)                            294

Stafu Sajini wa Magereza  (S’SGT)                      1599

Na waliohudhuria mafunzo katika vyuo vya Magereza vya Ukonga ­­– Dar es Salaam, KPF – Morogoro na Kiwira – Mbeya walikuwa kama ifuatavyo:-

Warakibu Wasaidizi wa Magereza  (ASP)                              136

Wakaguzi Wasaidizi wa Magereza  (A’INSP)                       1536

Maafisa Wateule wa Magereza  (RSM)                                   30

Sajini wa Magereza  (SGT)                                                      2362

Koplo wa Magereza  (CPL)                                                     2518

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, idadi hiyo ya upandishwaji vyeo kwa wakati mmoja haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza mnamo mwaka 1931.

Aidha, upandishwaji huo wa vyeo umeenda sambamba na urekebishaji wa mishahara yao kwa wakati hivyo kuondoa tatizo la ucheleweshaji wa marekebisho ya mishahara kwa watumishi hao.

 • Kulipa malimbikizo ya mishahara

 Ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imeweza kulipa malimbikizo ya mishahara (salary arrears) kwa maafisa na askari 515. Malimbikizo hayo yalitokana na kutorekebishiwa mishahara yao kwa wakati katika siku za nyuma baada ya kupandishwa vyeo mbalimbali.

 • Nishani

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ametunuku nishani mbalimbali kwa maafisa na askari wa Jeshi la Magereza, nishani hizo ni za Utumishi Uliotukuka 50, Utumishi wa Muda Mrefu na Tabia Njema 50 na nishani 05 za Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Kuimarisha majengo na miundombinu ya Jeshi la Magereza:

 

 • Ofisi za Makao Makuu ya Magereza –Dodoma

Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Samia Suluhu Hassan, Jeshi la Magereza limekamilisha ujenzi wa Ofisi yake ya Makao Makuu katika eneo la Msalato jijini Dodoma ambao umegharimu kiasi cha Shilingi 2,400,000,000 kazi zilizofanyika ni kukamilisha majengo ya ofisi za divisheni ya fedha na mipango, sheria na uendeshaji wa magereza, ukumbi wa mikutano, jiko na mgahawa, uzio wa ukuta kuzunguka makao makuu, kuchimba kisima cha maji cha kisasa pamoja na kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 130,000 za maji na kufanya usanifu wa mazingira (landscaping), kazi ambazo hazijakamilika lakini ujenzi wake unaendelea ni ukumbi mkubwa wa mikutano uliopo pembezoni mwa barabara ya Arusha na ujenzi wa barabara (pavements).

 • Ujenzi wa Hospitali ya Jeshi la Magereza Ukonga Dar es Salaam

Hii ni Hospitali kubwa kabisa ya Jeshi la Magereza iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam ambayo ujenzi wake ulianza zaidi ya miaka minne iliyopita. Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita ujenzi wake umefikia hatua nzuri na hivi karibuni uliwekewa jiwe la msingi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh, George B. Simbachawene (Mb) ambaye kwasasa ni Waziri wa Sheria na  Katiba, baadhi ya huduma zinazopatikana katika hospitali hiyo ni matibabu ya nje (OPD), maabara, huduma ya mama na mtoto (RCH), upimaji wa Virusi vya Ukimwi na ushauri (CTC), ultra sound, chanjo ya UVIKO- 19 na huduma ya meno. Hadi hivi sasa gharama za ujenzi wa hospitali hiyo zinakadiriwa kufikia shilingi 1,438,568,568.

Aidha, kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DMO) Hospitali hii imepokea kiasi cha shilingi 300,000,000 kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya kutolea huduma za afya ya msingi kwenye Serikali za Mitaa kupitia mpango maalum wa “Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19” fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo ujenzi wa jengo la kutolea huduma za dharura (Emergency Medicine Department) linajengwa. Pindi itakapokamilika, hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 300 kwa wakati mmoja huku wanufaika wakubwa wakiwa maafisa, askari, wafungwa/ mahabusu pamoja na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

 • Ujenzi wa Makazi ya Watumishi

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza linaendelea kukamilisha ujenzi wa nyumba 119 za kisasa za kuishi maafisa na askari katika maeneo mbalimbali ya magereza hapa nchini, nyumba hizi zina uwezo wa kuchukua familia 210. Ujenzi wa nyumba hizo ambao mpaka sasa umegharimu kiasi cha shilingi 7,280,000,000 upo katika hatua za ukamilishaji (finishing).

 

 • Ujenzi wa Gereza Karatu

Hili ni gereza jipya kabisa kujengwa katika wilaya hii ambayo hapo awali haikuwa na gereza, ujenzi wa gereza hili umeenda sambamba na ujenzi wa nyumba tatu za kuishi watumishi wa gereza hilo ambapo uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wake ulifanyika Novemba 15, 2021 na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo Mh, George B. Simbachawene (Mb), ujenzi wa Gereza hili ambao kwasasa umefikia hatua ya lenta umegharimu kiasi cha shilingi 280,000,000.

 • Ukarabati wa Gereza Mkono wa Mara Morogoro

Katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limeweza kufanya ukarabati mkubwa wa mabweni ya kulala wafungwa sambamba na ujenzi wa jengo la utawala na ukuta wa ngome ya Gereza Mkono wa Mara mkoani Morogoro. Ukuta huo upo katika hatua ya ukamilishwaji.

 • Ujenzi wa Gereza Kilosa

Serikali imeanza ujenzi wa gereza jipya kabisa na la kisasa katika wilaya ya Kilosa. Ujenzi wa gereza hili ambao utagharimu zaidi ya shilingi 400,000,000 kwa sasa upo katika hatua ya msingi na unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi sita.

 • Ujenzi wa ukuta wa ngome Gereza Mbigiri, Idete, Kwitanga

Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limeendelea kukamilisha ujenzi wa ukuta wa ngome ya Gereza Mbigiri, Idete na Kwitanga.

 • Ujenzi wa Hospitali kubwa ya Jeshi eneo la Veyula Dodoma

Jeshi la Magereza limeanza ujenzi wa hospitali kubwa ya Jeshi eneo la Veyula Mkoani Dodoma. Ujenzi wa hospitali hii ambao uko katika hatua ya msingi umeanza na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na mara itakapoamilika itakuwa ni msaada mkubwa kwa maafisa na askari na wananchi wanaozunguka eneo hilo kwa ujumla.

 • Ujenzi wa Zahanati ya Msalato

Hii ni zahanati iliyopo Gereza Msalato jijini Dodoma ambayo ilizinduliwa rasmi Agosti 27, 2021 na Mkuu wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee. Huduma zinazotolewa katika zahanati hii ni pamoja na huduma ya mama na mtoto (RCH), ushauri nasaha na upimaji wa Virusi vya Ukimwi, maabara, utoaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili. Wanufaika wakubwa wa zahanati hii ni pamoja na maafisa, askari, wafungwa pamoja na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Maboresho katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani:

 • Ukamilishaji wa Kiwanda cha Samani – Eneo la Msalato

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imeliwezesha Jeshi la Magereza kukamilisha ujenzi wa Kiwanda cha Samani kilichopo eneo la Msalato jijini Dodoma kwa kuweka miundo mbinu ya umeme, maji safi na majitaka, kufanya usanifu wa mazingira (landscaping) pamoja na kununua na kufunga mashine za kutengeneza samani. Kazi zingine zilizofanyika ni pamoja na umaliziaji (finishing) kwa kuweka sakafu, lipu na rangi.

 • Ujenzi wa Kiwanda cha Maziwa Mtego wa Simba –Kingolwira

Jeshi la Magereza kupitia Shirika la Magereza limejenga Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Maziwa katika Shamba la Magereza Kingolwira, Kiwanda hiki kinachangia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuzalisha ajira kwa wazalishaji wa maziwa wanaozunguka eneo la kiwanda, kuchangia pato la taifa, pamoja na kuboresha afya za wananchi, Kiwanda hiki kilizinduliwa rasmi Oktoba 15, 2021 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ally Mwinyi. Aidha, uzinduzi wa kiwanda hiki ulienda sambamba na uzinduzi wa Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto cha gereza hilo.

            (c ) Ujenzi wa Kiwanda cha Kuoka Mikate cha Msalato

Katika kipindi cha Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limefanikiwa kuanzisha mradi wa Kiwanda cha Kuoka Mikate kilichopo kandokando ya barabara ya Arusha eneo la Msalato jijini Dodoma.

 Kiwanda hiki ambacho kiliwekewa jiwe la msingi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo Mh, George B. Simbachawene Septemba 1, 2021 kilianza rasmi uzalishaji Desemba 20,2021 huku bidhaa zinazozalishwa Kiwandani hapo zikiwa ni mikate, skonzi, maandazi na keki.

Wateja wakubwa wa bidhaa hizo ni watu binafsi wa maeneo ya Namanga, Veyula, Msalato, Mipango pamoja na Gereza Isanga na watumishi wa Makao Makuu ya Magereza.

 • Ujenzi wa Kituo cha Biashara Isanga

Huu ni mradi mkubwa kabisa wa biashara ambao uko eneo la Isanga jijini Dodoma. Mradi huu ambao unahusisha ukumbi mkubwa wa sherehe, maduka ya biashara, sehemu ya kuoshea magari (car wash), sehemu ya maonyesho ya bidhaa (show room) na sehemu ya kuchezea watoto ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi 500,000,000 uliwekewa jiwe la msingi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. George B. Simbachawene (Mb) Agosti 17, 2021.

Kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo:

 

 • Mradi wa umwagiliaji Gereza Idete na ghala la kuhifadhia mazao

Huu ni moja ya miradi mikubwa kabisa ya kimkakati ya Jeshi la Magereza ambao ulianzishwa kwa malengo ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji mwaka 2013, kutokana na mkandarasi kutokuwa na kasi inayoridhisha Jeshi la Magereza liliiomba Wizara iukabidhi mradi huo kwa wataalamu wake toka kwa mkandarasi ili uweze kukamilishwa na kufikia malengo ya uanzishwaji wake.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ya mradi huo kwa hatua ya kufikisha maji shambani. Kazi inayoendelea ni kukamilisha miundombinu ya kusambaza maji shambani katika ekari 200. Kwa ujumla mradi huu unaendelea vizuri.

 Awamu ya tatu ya mradi huu ni kusambaza maji shambani kumalizia eneo lote la ekari 1000 za kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga na mara utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 975 kwa mwaka.

Mradi huo ambao hadi kufikia hapo umegharimu shilingi 4,000,000,000 umewekewa jiwe la msingi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh, Jumanne Sagini (Mb) Januari 29, 2022.

Aidha, ujenzi huo wa mradi wa umwagiliaji umeenda sambamba na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao ya nafaka ambao umegharimu zaidi ya shilingi 300,000,000 Ghala hili lina uwezo wa kuhifadhi mazao hadi tani 600.

 

Kuimarisha Kikosi cha Ujenzi cha Magereza:

Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limefanikiwa kuimarisha kikosi chake cha ujenzi kwa kununua malori matano (05) ya tani kumi yenye thamani ya zaidi ya shilingi 500,000,000 aidha, jeshi limenunua pia mtambo maalumu wa kuchimba visima uliogharimu shilingi 550,000,000.

Kwa ujumla katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Jeshi la Magereza limepata mafanikio makubwa, hii ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa miradi yake kwa kasi kubwa, hivyo kuakisi kauli mbiu ya Serikali ya kazi iendelee.