DODOMA. Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleimani Mzee Leo Tarehe 11 Machi 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Dkt. Francis Lutalala, ambaye ni Mratibu wa Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa(CHF) Jijini Dodoma kwa lengo la kuona  uwezekano wa  kuboresha afya ya Watumishi wa Jeshi hilo pamoja na Wafungwa na Mahabusu waliopo Magerezani.

 
Jenerali Mzee amesema kuwa amefurahishwa na ujio wa Dkt. Lutalala, kwakuwa umetoa mwangaza kuelekea mpango wa kupunguza gharama za matibabu kwa Wafungwa kutokana na bima hiyo kuchukua watu Sita kwa gharama nafuu ya Shilingi Elfu 30 kwa mwaka, huku akiweka wazi nia yake ya kujenga Hospitali kubwa katika eneo la Msalato yalipo Makao Makuu ya Jeshi Hilo.
 
''Niseme tu nimefurahishwa na ujio wako, hii bima nimekubaliana nayo na Nina mpango wakujenga hospitali kubwa kwahiyo ninaimani Mambo yataenda vizuri na tutaboresha zaidi Afya za watu wetu"
 
Kwaupande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Gereza Msalato Dkt. Mpamba Juma amesema, wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi wa maeneo ya jirani pamoja na Wafungwa kwa kushirikiana na CHF.
 
''Sisi tumejipanga vizuri Sana katika kutoa huduma, hivyo kuja kwa CHF kutapelekea huduma kuwa Bora zaidi kwakuwa wanachi wengi Sasa wenye bima hii wataanza kuja katika Zahanati yetu'' alisema Mpamba.
 
Akizungumzia mafanikio ya ujio wake Dkt. Lutalala mratibu wa CHF amesema, anashukuru kukutana na Jenerali Mzee na kufanya nae mazungumzo chanya, ambapo amemueleza namna walivyo itangaza Zahanati ya Gereza Msalato na Mafanikio yanayoanza kuonekana kwa muda mfupi, huku akiahidi kulichukua wazo la kujenga Hospitali kubwa zaidi na kulifikisha kwa Mkuu wa Mkoa ili kupata msaada zaidi.