Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma

SERIKALI imeridhishwa na kiwango cha kazi zinazofanywa na Bodi ya Taifa ya Parole pamoja na Bodi za Parole mikoa katika utekelezaji wa Sheria ya Bodi ya Parole nchini licha uwepo wa changamoto mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhe. Hamad Masauni (Mb) katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya Taifa ya Parole iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, leo Mei 14, 2020 jijini Dodoma ambapo amewataka kutekeleza wajibu wao ipasavyo kama Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyowaamini na kuwapa jukumu hilo.

“Serikali inaridhishwa sana na kiwango cha kazi mnazozifanya kikamilifu katika urekebishaji wa wahalifu kwa kuwapa wafungwa fursa ya kutumikia sehemu ya adhabu zao wakiwa nje ya magereza kwa usimamizi wa jamii nzima. Hongereni sana”, amesema Naibu Waziri Masauni.

Waziri Masauni amesema kuwa ustarabu wa nchi zote duniani hupimwa kwa kuzingatia namna zinavyoshughulikia uhifadhi salama na urekebishaji wa wahalifu katika magereza.

Aidha, ameongeza kuwa nyenzo kubwa ya msingi zitakazowawezesha wajumbe wa Bodi hiyo ni kujenga uewelewa wa mpango wa Parole , uelewa wa dhana na filosofia yake na umhimu wake katika jamii.

“ Ni muhimu sana ninyi wajumbe wa bodi hii ya Taifa Parole kuielewa sheria yenyewe na taratibu zake kiutekelezaji, dhana yenyewe, filosofia ya mpango wa Parole na manufaa yake katika jamii”, amesisitiza Naibu Waziri Masauni.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Masauni amewaasa wafungwa wote wa Parole nchini ambao wamenufaika na utaratibu huo kuwa na nidhamu na washirikiane vema na jamii inayowazunguka ili kudhihirisha kwamba wamebadilika tabia na kuaacha uhalifu

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa Parole, Dkt. Augustino Mrema amesema kuwa atahakikisha kuwa anafanya kazi kwa weledi mkubwa huku akishirikiana na wajumbe wote na atahakikisha bodi hiyo inasonga mbele na si kurudi nyuma. Aidha, ametoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo.

“Napenda nitoe shukrani zangu za kipekee kwa Rais Magufuli kwa kuniteua kwa mara nyingine kuiongoza bodi hii, kuteuliwa kwangu ni ishara ya imani katika kulibeba jukumu hili la kijamii”, amesema Mwenyekiti Parole Taifa, Dkt. Mrema.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Suleiman Mzee ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Taifa Parole amempongeza Mhe. Dkt. Augustino Mrema kwa kuteuliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa Parole pamoja na wajumbe wote na kuongeza kuwa hiyo inadhihirisha imani kubwa ya Serikali katika kubeba dhamana hiyo.

Kamishna Jenerali Mzee amesema kuwa tangu bodi hiyo ya Parole Taifa ianze kutekeleza Sheria ya Parole nchini mpaka sasa wamefanikiwa kujadili wafungwa 6,237, wafungwa walionufaika kwa Parole ni 5,535, na wafungwa waliokataliwa kwa sababu mbalimbali 702. Aidha, mpaka sasa ni wafungwa 25 tu ndio waliokiuka masharti ya Parole na kurudishwa magerezani.

“Mhe. Naibu Waziri mpaka sasa jumla ya vikao 41 vimeshafanyika tangu ianzishwe Sheria ya Bodi za Parole nchini na imewezesha kujadili wafungwa hawa walionufaika na wale ambao hawakunufaika”, amesema Kamishna Jenerali Mzee.

Bodi ya Taifa Parole ni tasnia muhimu sana katika urekebishaji wa wahalifu kwa kuishirikisha jamii. Tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo mwaka 1994 mafanikio makubwa yameonekana kutokana na baadhi ya wafungwa kuachiliwa kupitia utaratibu huu hivyo kupunguza sehemu ya changamoto ya msongamano magerezani. Kwa habari picha Zaidi tembelea magereza blog