Na ASP. Lucas Mboje, Moshi

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama leo ametembelea na kukagua ujenzi wa majengo ya Kiwanda kipya cha bidhaa za ngozi kinachojengwa katika eneo la Gereza Kuu Karanga, Moshi na kuridhishwa na hatua kubwa zilizofikiwa.

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo wa ubia kati ya Jeshi la Magereza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF upo katika awamu ya kwanza na hivi sasa umefikia asilimia 60 ya ujenzi wa majengo yote manne ambapo unatarajiwa kukamilika Machi 2, 2020 hivyo, kuwezesha ufungaji wa mashine mbalimbali za kiwanda hicho.

“Nimefarijika sana kwa hatua zilizofikiwa za ujenzi, leo Makamanda kwa kweli niwapongeze kwa kazi hii endeleeni kusimamia ujenzi huu kwa kasi kwani kiwanda hiki kina umuhimu mkubwa kwa upande wa serikali na manufaa ya kiwanda hicho ni ya kiuchumi,” amesema Mhagama.

Waziri Mhagama aliongezea kuwa, adhma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinakamilika mapema kwani kina manufaa makubwa kwa taifa ikiwemo kutoa fursa nyingi za ajira kwa watanzania pamoja na kuongeza mapato serikalini.

Aidha, Waziri Mhagama amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Andrew Massawe kuhakikisha kuwa anaandaa mpango kazi wa utekelezeji wa mambo yote muhimu yanayohusiana na kiwanda hicho ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mara baada ya ujenzi wake kukamilika.

“Tunapoendelea na ujenzi wa kiwanda hiki cha bidhaa za ngozi ni lazima twende sambamba na mambo mengine muhimu ikiwemo upatikanaji wa maji ya kutosha katika kiwanda hiki, usimikaji wa miundombinu ya umeme pamoja na kufanya maandalizi ya masoko ya bidhaa zitakazokuwa zikizalishwa na kiwandani”, amesisitiza Mhagama.

Kwa upande wake Mhandisi wa mradi huo, Mrakibu wa Magereza, Julius Sukambi amesema kuwa utekelezaji wa mradi unafanyika usiku na mchana kwa kutumia wataalam wa Jeshi la Magereza, wafungwa na mafundi raia wa fani mbalimbali ikiwa ni jitihada za kuwezesha kukamilisha mradi huo kama ilivyokusudiwa.

 

Hatahivyo, Mhandisi huyo, Mrakibu wa Magereza, Julius Sukambi amemhakikishia Mhe. Mhagama kuwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa ifikapo Machi 2, 2020.

 

Januari 15, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alitembelea mradi huo ambapo katika ziara hiyo, Waziri Mhagama alimuagiza Mkandarasi wa mradi kuongeza kasi ya ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la Gereza Kuu Karanga, Moshi ili kiweze kukamilika kama ilivyokusudiwa.