Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike akizungumza katika kikao na Maafisa na askari wa vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na mikakati mbalimbali ya Jeshi ikiwemo ya Kilimo, viwanda na ufugaji. Kikao kazi hicho kimefanyika Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.

 

Na ASP Lucas Mboje, Jeshi la Magereza;

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amewaasa Maafisa na askari wote wa Jeshi hilo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia nidhamu ya kazi na kufuata taratibu zilizopo ndani ya Jeshi.

Amesema hayo jana katika kikao kazi na Maafisa na askari wa vituo vya Magereza Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya utendaji kazi, maadili ya kazi, nidhamu na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Jeshi hilo ikiwemo mpango mkakakti wa kilimo, uwekezaji katika viwanda na ufugaji.

Kamishna Jenerali Kasike amesisitiza kuwa nidhamu ni muhimu Jeshini na amesema hakuna mtu aliye juu ya nidhamu kwani msingi wa Jeshi lolote lile ni nidhamu.

"Taswira ya Jeshi la Magereza inategemea zaidi utekelezaji mzuri wa majukumu yenu kwa kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi. “Kila mmoja lazima atimize wajibu wake kikamilifu kwa kutumia uweledi, ubunifu na kuzingatia nidhamu ya kazi”, alisisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa wapo baadhi ya maafisa na askari ambao wanamatatizo ya kinidhamu na hawataki kubadilika hali ambayo inaharibu taswira ya Jeshi hilo katika jamii.