Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitembelea maeneo ya mji wa Serikali Ihumwa, jijini Dodoma yanapojengwa majengo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana na Walemavu, leo januari 31, 2019.

 

Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma


KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike leo januari 31, 2019 ametembelea maeneo ya mji wa Serikali Ihumwa, jijini Dodoma yanapojengwa majengo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana na Walemavu ambapo amekiagiza Kikosi cha ujenzi cha Jeshi la Magereza kinachoshiriki katika ujenzi wa ofisi hizo kuzingatia ubora katika ujenzi wa majengo hayo.

Kamishna Jenerali Kasike amewataka pia Maafisa na askari wanaoshiriki katika ujenzi wa ofisi hizo  kuongeza kasi ya ujenzi kama ambavyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivyoagiza lakini wazingatie viwango vya ubora katika ujenzi huo.

"Hakikisheni ujenzi unafanyika usiku na mchana kama tulivyokwishajipanga lakini zingatieni viwango vya ubora katika ujenzi". Amesisitiza Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amemtaka Msimamizi Mkuu wa Kikosi cha Ujenzi cha Magereza katika mradi huo, ACP. Aron Lunyungu pamoja na Mhandisi Mradi, SSP. Alfred Bundala kuhakikisha kuwa wanakusanya mahitaji yote muhimu katika eneo la ujenzi ili kufanikisha kasi ya ujenzi huo.

Ujenzi wa majengo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi ulitarajiwa kukamilika mapema ifikapo tarehe 31 Januari 2019 lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa nje ya uwezo wa Kikosi cha ujenzi cha Jeshi la Magereza, ujenzi huo umechelewa kukamilika kwa wakati na hatua za ukamilishaji zinaendelea kwa kasi ya kuridhisha.