Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Gereza Kitete – Nkasi, SP. Job Lwesya(wa kwanza kulia) alipotembelea Gereza hilo leo Januari 27, 2019 kwa kwa lengo la kukagua mashamba ya maharage. Gereza hilo limepewa malengo ya kulima hekari 300 za zao la maharage ambapo hadi sasa limekwishalima hekari 114 na mandalizi ya kulima mashamba mengine ili kufikia malengo hayo yanaendelea.

 

Na ASP. Lucas Mboje, Nkasi
KATIKA kuelekea kwenye mpango wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani Gereza la Kilimo Kitete – Nkasi limeanza uzalishaji wa maharage ambapo katika msimu huu wa mwaka 2018/2019 tayari limelima zao hilo.

Akizungumza leo mara baada ya kutembelea Gereza hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa ameridhishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea katika kufanikisha mpango mkakati wa uzalishaji wa chakula kwa wingi katika maeneo yakimkakati pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa na vitendea kazi.

“Ni lazima tuhakikishe kuwa jukumu hili tulilopewa linatekelezwa ipasavyo hivyo, Mkuu wa Gereza pamoja na timu yako hakikisheni mnaongeza bidii ya kazi kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa ili kufikia malengo ya hekari 300 za zao la maharge mlizopewa kwani msimu bado unaruhusu”. Alisema Kamishna Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa Jeshi litaangalia uwezekano wa kuliwezesha Gereza Kitete zana mbalimbali za kilimo kama vile trekta, ambazo zitarahisisha kufanikisha malengo ya kimkakati ili kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa.

Ameongeza kuwa Gereza Kitete - Nkasi ni miongoni mwa magereza 10 ya kimkakati ambayo tayari yameainishwa katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa. Magereza mengine ni Songwe, Mollo, Arusha, Idete, Kiberege, Kitengule, Pawaga, Kitai na Gereza Ludewa.

Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali Kasike amewaasa viongozi wa Jeshi hilo pamoja na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia vitengo(Ugavi na Uhasibu) katika vituo vyao kuzingatia suala la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo vyote vya ubadhilifu wa mali za umma ili kuwezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kitete, SP. Job Lwesya alisema kuwa  katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2018/2019 gereza hilo limelima ekari 114 za maharage na kwa sasa linaendelea na maandalizi ya mashamba mengine ili kufikia malengo waliyopewa ya kulima hekari 300 za maharage.

Aidha, aliongeza kuwa  gereza hilo linayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba hivyo wamejipanga kimkakati katika kuhakikisha kuwa wanazalisha mazao mbalimbali kwa wingi kwa ajili ya chakula wafungwa.

Gereza Kitete - Nkasi lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3,742 ambazo zinafaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula ikiwemo zao la maharage, mahindi na Arizeti.

Gereza hilo lilianzishwa rasmi mwaka 1989 kwa lengo la kuwahifadhi wahalifu pamoja na kuwapatia wafungwa programu za urekebishaji ili wamalizapo vifungo vyao waweze kuwa raia wema.