Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Augustino Mrema(kushoto) akiongoza kikao cha kujadili Wafungwa waliopendekezwa kunufaika/kutonufaika katika mpango wa Parole. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ambaye pia ni Katibu wa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole. Kikao hicho cha siku mbili  kimefanyika leo Oktoba 13, 2018, katika Bwalo la Gereza Kuu Isanga, Jijini Dodoma.

 

Na Lucas Mboje, Dodoma;

Kikao cha 39 cha Bodi ya Taifa ya Parole kimeanza leo  Oktoba 13, 2018 chini ya Uenyekiti wa Mhe. Augustino Mrema katika Ukumbi wa Gereza Kuu Isanga, Jijini Dodoma.

Kikao hiki cha siku mbili  kwa mujibu wa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole kitajadili Wafungwa waliopendekezwa kunufaika/kutokunufaika katika mpango wa Parole.

Utaratibu huu wa Parole hapa nchini ni mojawapo ya adhabu mbadala wa kifungo ambao ni matokeo ya mfumo uliobuniwa na jamii katika nchi nyingi ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza ongezeko la wafungwa ndani ya magereza hivyo kuipunguzia Serikali na wananchi ambao ndio walipa kodi mzigo mkubwa wa kuwahudumia wafungwa wawapo magerezani.

Lengo Kuu la Sheria ya Bodi ya Parole ya Mwaka 1994 ambayo ilifanyiwa marekebisho Mwaka 2002 ni kuweka masharti maalum kuhusu utaratibu wa urekebishaji wa wahalifu nje ya kuta za magereza baada ya Mfungwa kutumikia sehemu ya kifungo chake na kuonesha mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na Kanuni zake.

Pamoja na utekelezaji wa Sheria hii hapa nchini  kumekuwepo  na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wake ikiwemo  ufinyu au wigo mdogo wa kisheria uliowekwa na Sheria yenyewe ambapo kutokana na wigo mdogo uliopo wa kisheria takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wafungwa wengi hawawezi kujadiliwa kwa kuwa hawana sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria iliyopo.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo mfungwa anayestahili kunufaika na mpango wa Parole ni yule anayetumikia kifungo cha miaka minne(4) na kuendelea na awe ametumikia theluthi moja (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na Kanuni zake.

Hiki ni Kikao cha 5  kufanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Augustino Mrema  tangu ateuliwe na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole Julai 16, 2016.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com