Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Magereza mara baada ya kuwasili katika Gereza la Wilaya Singida leo Agosti 23, 2018 tayari kwa ziara yake ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo Mkoani Singida.

(Picha na Jeshi la Magereza)

 
Na Lucas Mboje, Singida;

MKUU wa Jeshi la Magereza nchini – CGP Phaustine Kasike ameonya vikali tabia ya maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wanaojihusisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwani kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za uendeshaji wa Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali Kasike amesema hayo leo Alhamisi katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo Magereza Mkoani Singida.

Amesema kuwa limezuka wimbi la askari wa Jeshi hilo kutumia vibaya mitandao ya kijamii kinyume na maadili ya Jeshi hilo kwa baadhi ya askari kuitumia vibaya kuchangia na kutoa maoni katika mitandao ya kijamii mambo yasiyofaa.

Jenerali Kasike  amewataka askari wote nchini kuepuka kulichafua jeshi hilo mbele ya jamii badala yake wanatakiwa kuwa kielelezo kwa Taifa.

“Niwasihi sana jiepusheni na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii bali itumieni kupashana habari za msingi na zenye manufaa kwenu kwani nafahamu mitandao ya kijamii inarahisisha kupashana habari kwa uharaka zaidi.” Alisisitiza Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna  Jenerali Kasike ameongeza kuwa Jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu askari yeyote atakayebainika kutenda makosa hayo ya kimaadili kwani yanalifedhehesha Jeshi la Magereza mbele ya jamii.

Kuhusu upungufu wa nyumba za kuishi kwa watumishi wa Jeshi hilo, Jenerali Kasike amewataka wakuu wote wa magereza nchini kuwa wabunifu hususani katika kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ikiwemo fursa ya kufyatua tofali za kuchoma ili kupunguza tatizo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Kilimo na Mifugo Ushora, Mrakibu wa Magereza Kulwa Kabota ameushukru Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kuwawezesha kiasi cha Shilingi Milioni 9 ambazo zitasaidia kukamilisha ujenzi na upauaji wa nyumba ya askari katika gereza hilo.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike yupo katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Singida ambapo amekagua Gereza la Wilaya Singida na Gereza la Kilimo na Ufugaji Ushora kabla ya kuelekea jijini Dodoma kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogpsot.com