Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike akipokea salaam ya heshima kutoka kwa gadi maalum iliyoandaliwa kwa ajili yake alipofanya ziara ya kiazi leo Agosti 13, 2018 katika gereza la Isanga mkoani Dodoma.

Picha na Jeshi la Magereza

 

Na Deodatus Kazinja

Watendaji wote ndani ya Jeshi la Magereza wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kupokea mkakati maalum wa uzalishaji wa chakula unaolenga kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na ziada kuuzwa katika sehemu nyingine.

Hayo yamesemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Phaustine Kasike leo Agosti 13, 2018 alipokuwa akizungumza na maafisa, askari na watumishi raia wa jeshi hilo alipofanya ziara yake ya kwanza mkoani Dodoma tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Julai 13 mwaka huu.
Kamishna Jenerali Kasike amesema maandalizi ya mkakati huo yanaendelea vizuri makao makuu ya jeshi hilo na katika kipindi kifupi kijacho maelekezo ya utekelezaji wake yatatolewa na kushushwa katika vituo vyote vya magereza kwa ngazi ya mikoa na wilaya.

Amesema mkakati huu utakapokuwa umekamilika itakuwa ndiyo dira ya utekelezaji ndani ya jeshi na utamtaka kila kiongozi kuwa na mpango kazi katika eneo lake unaokwenda sambamba na malengo mapana ya jeshi hilo.

“Ninaamini jambo hili linawezekana na kwa kuanza na raslimali chache zilizopo kwakuwa wataalam wapo, ardhi ipo na nyenzo za kuanzia zipo tukijipanga vizuri tunaweza kupata mahala pazuri pa kuanzia” Amebainisha Jenerali Kasike

Na kuongeza “ miongoni mwa taasisi zenye wasomi wazuri katika maeneo mengi ni pamoja na jeshi letu la Magereza, sasa umefika wakati wa kuona wataalam hawa wanatumika kwa kushirikikshwa ipasavyo ili kuona wanaleta tija jeshini na taifa kwa ujumla”

Sanjari na hayo Kamishna Kasike amewataka watumishi wa jeshi hilo kote nchini kubadili mtazamo wa namna wanavyofanya kazi kwa kusoma alama za nyakati na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kamishna Kasike amesema ifike mahala kila mmoja ajisikie aibu na fedheha kuona jeshi letu linasemwa vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hata katika mambo ambayo yako ndani ya uwezo wa watendaji wenyewe.

Akitolea mfano wa uingizwaji wa vitu visivyoruhusiwa magereza kama vile simu, bangi, pesa nakadhalika kutohitaji bajeti kuviondoa ni kiasi cha watendaji kubadilika tu.

“ Hapa kuna tatizo kubwa la kimaadili, badilikeni. Nitakuwa mkali sana. Nimeanza kwa kuwaeleza ili nieleweke vizuri kwa hatua nitakazozichukua kwa askari asiyetaka kubadilika. Adhabu zitakuwa kali kwelikweli. Amesisitiza Jenerali Kasike.

Amewakumbusha askari wote nchini kutambua dhamana waliyonayo, thamani ya kazi yao na dhamana walizonazo kwa familia zao ili kuachana na tamaa zisizokuwa na msingi ambazo mwisho huwaingiza katika matatizo makubwa.

Aidha, Kamishna Kasike amewaambia kuwa anatambua uwepo wa changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa nyumba na zilizopo kuchakata, ukosefu mkubwa wa vyombo vya usafiri, malimbikizo ya madeni, kutopandishwa vyeo kwa wakati, uhaba wa sare na mengine.

Amewahakikishia kuwa serikali iliyoko madarakani inayatambua yote na tayari imeanza kuchukua hatua katika baadhi ya mambo na kuwaomba ushirikiano wakati yeye akiwa mtendaji mkuu anafanya ufuatiliaji.

Ziara ya Kamishna Kasike mkoani Dodoma imemfikisha pia gereza Msalato ambapo ametembelea mradi wa upigaji kokoto na kuzungumza na maafisa na askari wa gereza hilo. Awali alimtembelea Katibu Mkuu Utumishi Dr.Laurean Ndumbaro ofisini kwake na kubadilisha taarifa mbalimbali za kiutendaji.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com