Na Lucas Mboje, Magereza;

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amewataka Maofisa na askari wa Jeshi hilo kujiepusha na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya kazi yao, badala yake wazingatie kanuni, miiko na maadili ya uendeshaji wa Jeshi la Magereza.

Kamishna Jenerali Kasike ametoa rai hiyo jana Agosti 1, 2018 wakati akiongea na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoani Arusha alipofanya ziara ya kikazi Mkoani humo.

Alisema kuna upungufu katika uzingatiaji wa maadili kwa baadhi ya Maofisa na askari hususani mahusiano mabaya ya askari na wafungwa ikiwemo tabia za askari kuingiza simu magerezani.

Amesema hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa maofisa na askari watakaobainika kufanya vitendo hivyo ikiwemo kuwajibishwa na kufukuzwa kazi.

"Mnajua kabsaa gharama za kujihusisha na tabia hizi za mahusiano mabaya na wafungwa nawaasa mzingatie maadili mnapotekeleza majukumu yenu ya kazi". Alisisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Kuhusu agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa Kamishna Jenerali Kasike amesena kwa sasa Jeshi hilo linakamilisha mpango kazi wake utakaowezesha utekelezaji wa agizo hilo.

Amewataka askari wote nchini kujiandaa kisaikolojia kutekeleza agizo hilo bila kisingizio chochote kwani Jeshi la Magereza linazo rasilimali za kutosha kutekeleza agizo hilo.

"Tunayo ardhi yakutosha, nguvu kazi ya wafungwa ipo hivyo agizo la Rais na Amiri Jeshi Mkuu lazima litekelezwe bila kisingizio chochote". Alisema Jenerali Kasike.

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Arusha ambapo lengo la ziara hiyo ni kukagua utendaji kazi pamoja na kuzungumza na Maofisa na askari wa Jeshi hilo.