Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Flolens Luoga alipotembelea Benki Kuu ya  Tanzania katika ziara yake ya kujitambulisha kwa Viongozi waandamizi Serikalini leo Julai 25, 2018, jijini Dar es Salaam. 

(Picha zote na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Makao Makuu ya  Jeshi la Magereza).

 

Na Mwandishi wetu, Magereza

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kutoa mchango wake katika kudumisha hali ya ulinzi na usalama nchini kupitia majukumu yake ya uhifadhi salama wa wafungwa na utoaji wa huduma za urekebishaji kwani Amani na Usalama ni msingi wa maendeleo katika nchi yoyote duniani.

Prof. Luoga amesema hayo wakati wa mazungumzo katika ziara ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Phaustine Kasike alipotembelea Benki Kuu ya Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kujitambulisha kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa tangu ateulie kuwa Mkuu wa Jeshi hilo Julai13, 2018.

Aidha, Profesa Luoga amelishauri Jeshi la Magereza kuongeza ubunifu katika miradi ya uzalishaji mali kwa kufanya utafiti utakaoongeza ubora wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ili kuendana na mahitaji ya soko la ndani na hata nje ya nchi kwa kuwa taasisi kama magereza inaaminika.

“Jambo kubwa ni kubadili mtazamo na namna ya kufikiri kwa kusoma alama za nyakati na mabadiliko ya ulimwengu, kila kitu kinawezekana”. Amesisitiza Prof. Luoga.
Prof. Luoga ameahidi kuwa Benki Kuu ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Magereza hasa katika ushauri wa kitaalam pale itakapohitajika kufanya hivyo ili kufikia malengo mahususi.

Ameongeza kuwa Taasisi anayoiongoza italipa ushirikiano Jeshi la Magereza kwa kuliunganisha na wadau mbalimbali watakaofanya kazi na Jeshi hilo kufanikisha majukumu yake pale fursa za kufanya hivyo zitakapojitokeza.

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Kasike amekutana na Uongozi wa juu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Valentino Mlowola.

Mkurugenzi Mlowola amemhakikishia Kamishna Kasike ushirikiano wa dhati kwa kuwa vyombo hivyo viwili ni miongoni mwa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria nchini hivyo ukaribu wao katika utendaji hauepukiki.

“Msingi wa amani katika nchi umewekezwa katika vyombo vyetu, kwahiyo ushirikiano ni muhimu sana”. Amesema Mlowola.
Kamishna Jenerali Kasike yuko katika ziara ya kujitambulisha kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa ikiwa pia ni sehemu ya kuelezea majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ambayo ni pamoja na uhifadhi salama wa wahalifu na utoaji wa huduma za urekebishaji kwa wafungwa ili wawe raia wema pindi wamalizapo vifungo vyao.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com