Na Lucas Mboje, Jeshi la Magereza;

KAMISHNA Jenerali mpya wa Jeshi la Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Uongozi wake utaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa wafungwa wanazalisha chakula cha kutosha ili wafungwa waweze kujilisha magerezani.

Jenerali Kasike ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kupokelewa rasmi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa tayari mtangulizi wake alishaanza kuufanyia kazi mpango huo na amebainisha kuwa alipoishia mtangulizi wake ataanzia hapo ili mchakato huo ukamilike kwa ufanisi na hivyo kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli kuhusu wafungwa kuzalisha chakula chao wenyewe na hatimaye kujilisha.

Aidha, amewataka maofisa na askari wote wa Jeshi hilo nchini kuhakikisha kuwa wanabadilika kimtizamo na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea ili kuweza kutimiza matarajio na maelekezo mbalimbali ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli.

Pia, Kamishna Jenerali Kasike amesema watafanyia maboresho katika utaratibu wa kuwawezesha kiasi fulani cha fedha(Incentive scheme) wafungwa ambao wanaoshiriki moja kwa moja kwenye miradi ya uzalishaji mali ya Jeshi hilo ili kiasi hicho kiwawezeshe kuanzisha shughuli za kijasiriamali mara baada ya vifungo vyao huko uraiani.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa amempongeza Kamishna Jenerali mpya wa Magereza Phaustine Kasike kwa uteuzi huo na amemtakia kila la heri kwenye utekelezaji wa majukumu yake.