CGP Mteule DCP Phaustine M. Kasike, Alizaliwa mwaka 1965 na alipata Elimu ya Sekondari katika Shule ya Iyunga, Mbeya Mwaka 1984 na Elimu ya Kidato cha sita alihitimu katika Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro Mwaka 1987.

Alijiunga na Jeshi la Magereza katika Chuo cha Magereza Kiwira, Mbeya mwezi Mei, 1989 na kuhitimu Januari, 1990 ambapo alipata mafunzo ya awali ya uaskari Magereza.

Mwaka 1992 alipata mafunzo ya Uhusiano wa Kimataifa kwa ngazi ya Stashahada katika Chuo cha Diplomasia Tanzania, Dare s salaam. Mwaka 1999 alitunukiwa shahada ya kwanza ya Mahusiano ya Kimataifa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Mwaka 2015 alitunukiwa shahada ya Uzamili katika masuala ya Usalama na Stratejia katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Tanzania (NDC) Aidha, amehudhuria pia kozi inayohusu Usimamizi wa Utekelezaji wa Sheria (Law Enforcement) nchini Ghana mwaka 2006.

Katika utumishi wake ndani ya Jeshi la Magereza amepandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo Sajini wa Magereza(1990), Sajini taji wa Magereza(1993), Mkaguzi Msaidizi wa Magereza (1996), Mkaguzi wa Magereza (2001), Mrakibu Msaidizi wa Magereza (2005), Mrakibu wa Magereza (2008), Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (2010), Kamishna Msaidizi wa Magereza (2011), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (2017), Naibu Kamishna wa Magereza ( 2018).

Amewahi kufanya kazi katika nafasi ya Afisa Mafunzo Msaidizi Kitengo cha Mafunzo Makao Makuu ya Magereza (1990- 1991 na 1993 – 1995), Afisa Msaidizi Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa Makao Makuu ya Magereza wakati huo huo Msaidizi Mkuu wa Jeshi la Magereza (1999 – 2007).

Aidha, Mwaka 2007 – 2012 alihudumu katika nafasi ya Afisa Msaidizi Kitengo cha Usalama Makao Makuu ya Magereza, Afisa Mwelekezi Mwandamizi Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Tanzania (2013 - 2017), Mkuu wa Kitengo cha Parole (2017) na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (2018).

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Dar es salaam.

13 Julai, 2018.