Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kulia) akimvalisha cheo akimvalisha cheo Naibu Kamishna wa Magereza, Tusekile Mwaisabila kuwa Kamishina wa Magereza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga jijini Dar es salaam Juni  8, 2018.

 

Na Mwandishi wetu,

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, kwa niaba ya Amiri jeshi mkuu Rais John Magufuli amewavisha vyeo maafisa wa ngazi ya juu 9 wa Jeshi la Magereza waliopandishwa vyeo hivyo hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa maafisa 9 waliovishwa vyeo ni manaibu kamishna wa magereza - DCP wanne wa Jeshi hilo ambao wamepandishwa vyeo na kuwa Makamishna wa magereza, huku makamishna wasaidizi waandamizi wa Magereza -SACP watano wakipandishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna - DCP wa Jeshi hilo.

Waliovishwa vyeo kuwa Makamishna wa Magereza ni Naibu Kamishna wa Magereza Uwesu Ngarama, Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila, Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Urekebishaji, Naibu Kamishna wa Magereza Augustine Mboje, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Naibu Kamishna wa Magereza Gideon Nkana ambaye ni  Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam.

Wengine waliovishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna wa Magereza ni  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Julius Sang’udi, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Afwilile Mwakijungu, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, John Masunga, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Phaustine Kasike, Mkuu wa Kitengo cha Parole pamoja na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Jeremiah Katungu ambaye ni Katibu Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza.

Akizungumza mara baada ya kuwavisha vyeo Maafisa hao wa magereza(Ijumaa, Juni 8, 2018) katika hafla ya kuwavisha vyeo hivyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), Ukonga, jijini Dar es Salaam,  Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa amewataka makamishna hao wa Jeshi la magereza wa ngazi zote kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu  sambamba na kusimamia haki na usawa katika utekelezaji wa majukumu yao kila siku.

Aidha, Jenerali Malewa amemshukru Amiri jeshi mkuu Rais John Magufuli kwa kuwapandishwa vyeo maafisa hao ambao watajaza nafasi mbalimbali za juu za uongozi ndani ya Jeshi la Magereza kwani kwa muda mrefu safu ya juu ya uongozi ilikuwa na upungufu mkubwa wa kada ya maafisa wa vyeo hivyo hali iliyopelekea kuathiri utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Maafisa hao kabla ya kuvishwa vyeo hivyo walivyotunukiwa  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia Juni 02, 2018, walipata fursa ya kula kiapo cha Tamko la Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma mbele ya katibu wa sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com