PAROLE TANZANIA

1.0    HISTORIA YA PAROLE NCHINI TANZANIA                                       (Mitazamo ya Jamii kuhusu Parole)

Magereza nchini yalianzishwa Mwaka 1931 wakati wa utawala wa kikoloni kwa lengo la kutoa adhabu kwa wahalifu na kuijengea jamii hofu wasijiingize kwenye vitendo vya uhalifu. Ingawa mfumo huo wa Magereza ulilenga kulinda maslahi yao, ulikumbana na mvutano ulioufanya ubadilike na kwenda na wakati. Wafungwa wa enzi hizo walipewa kazi kama adhabu tu, kwa mfano kuchimba mitaro wakati wa kiangazi na kuifukia, au kupasua mawe na kuyafukia ardhini.

Baada ya Uhuru Taifa lilibadili falsafa ya Magereza kutoka ile ya utesaji na kukomoa, na kuwa ya urekebishaji wa wahalifu. Magereza yalianza kuboresha huduma magerezani, utu na heshima ya ubinadamu vilipewa kipaumbele na program mbalimbali kwa wafungwa zilizohusu mafunzo ya ujuzi wa stadi za kazi katika ufundi, kilimo na ufugaji na pia kuwapa ushauri nasaha wa kijamii, kisaikolojia na kiroho zilianzishwa. Hata hivyo ongezeko la watu,na kukua kwa teknolojia kulipelekea kukua kwa  uhalifu na  kulisababisha mambo makuu mawili yafuatayo:-

i.    Msongamano mkubwa wa wahalifu magerezani ulifanya uboreshaji wa huduma muhimu kama tiba, lishe, malazi na mavazi kutokidhi mahitaji.

ii.    Hofu na hisia kali katika jamii dhidi ya uhalifu na athari zake vilisababisha kwa namna fulani shinikizo kwa wanasiasa ambapo matokeo yake yalikuwa ni kutungwa kwa Sheria kali zilizoambatana na adhabu kali za vifungo virefu kwa wahalifu.

Adhabu ya kifungo kirefu ilionekana kama njia bora ya     kupambana na uhalifu. Hata hivyo, baada ya kipindi fulani athari zake zilianza kujitokeza kwa Serikali kushindwa kuwahudumia wafungwa ipasavyo kutokana na idadi yao kuwa kubwa.

Kwa mujibu wa Sheria na Sera za kitaifa kuhusu uboreshaji wa magereza zinazotolewa kufuatia kuridhiwa kwa maazimio mbalimbali ya Kimataifa katika kuboresha hali za wafungwa magerezani, imeonekana kuwa vifungo siyo njia pekee ya kumrekebisha mhalifu. Adhabu mbadala zimeonekana ni bora zaidi kuliko kifungo kwa vile jamii huhusishwa katika suala zima la kumrekebisha mhalifu. Aina za adhabu mbadala zinazotumika hapa nchini ni pamoja na kulipishwa faini, Kuachiliwa kwa masharti, Probation, Kuachiliwa kwa matazamio, Kifungo cha Nje (EML), Parole, Huduma kwa Jamii nk. Aidha, katika adhabu mbadala     zilizoainishwa, mpango wa Parole umeonekana unafaa zaidi kwa kuwa ndugu, uongozi wa mtaa/kijiji na mwathirika wa uhalifu hushirikishwa kutoa maoni kabla ya mfungwa husika kunufaika na mpango huu. Aidha, ni adhabu mbadala pekee inayohusika na wafungwa wanaotumikia vifungo virefu magerezani.

1.1    Maana ya Parole:
Parole ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa aliyehukumiwa kutumikia kifungo gerezani cha miaka minne na kuendelea kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada ya kukidhi vigezo vifuatavyo:

i).    Awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwenendo wa kurekebika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya kifungo chake kwa masharti maalum. Masharti hayo ni:
•    Kuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka atakapomaliza kifungo chake.
•    Kuzingatia masharti ya Parole anayopewa kikamilifu
•    Kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato halali katika jamii.
ii).    Awe ameonesha kujutia kosa, kurekebika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani.
iii).    Mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii.
 
Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani.  Utaratibu huu ni wa kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu ambao ndio wengi waliopo magerezani. Aidha, ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika urekebishaji kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni zao katika jamii.

1.2    Malengo ya kuanzishwa kwa Parole:
Madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu wa Parole  Nchini hayatofautiani na madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu huu kwenye nchi nyingine duniani zikiwepo nchi za Afrika kama vile: Afrika kusini, Zambia na Namibia.  Mfumo wa Parole ulioainishwa hapa nchini unatokana na uzoefu wa Parole unaotumika nchini Canada.  Sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa Parole hapa Nchini ni:-
i.    Kuhusisha jamii katika suala zima la urekebishaji wa wafungwa badala ya kutegemea serikali peke yake kwani chanzo cha uhalifu ni mazingira yanayotokana na jamii yenyewe.

ii.    Kuwepo na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wafungwa wenye vifungo virefu magerezani ambao kutokana na urefu wa vifungo vyao hawawezi kufaidika na programu zilizopo za urekebishaji kwa sababu ama watatoka magerezani wakiwa wazee wasiojiweza, watakutana na mabadiliko makubwa kijamii, kiuchumi na kisera wasiyoweza kuyamudu haraka/ipasavyo kwenda na wakati au watafia gerezani.  Wafungwa wa aina hii hukata tamaa kwani hawaoni sababu ya kuwa na nidhamu wawapo gerezani, hivyo kusababisha usalama magerezani kuwa mashakani.  Parole ilikusudiwa kuwarejeshea matumaini ya kurejea katika jamii na kuishi maisha ya kawaida na kupunguza tishio la kiusalama magerezani na katika jamii kwa ujumla.

2.0    KUTUNGWA KWA SHERIA YA BODI ZA PAROLE NCHINI
Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi liliwasilisha mapendekezo ya kutungwa Sheria ya Bodi za Parole nchini. Mapendekezo hayo yalijenga hoja ambayo hatimaye iliwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 1994 na kupitishwa rasmi kuwa Sheria ya Bodi za Parole Na. 25/1994. Sambamba na kutungwa kwa Sheria hiyo, kanuni za Bodi za Parole ziliandaliwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali tarehe 29 Agosti, 1997 (GN. 563/1997) hivyo kuwezesha Sheria hiyo kuanza kutumika rasmi. Hata hivyo Sheria iliyopitishwa haikuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Jeshi la Magereza ambayo yaliwalenga wafungwa wote kunufaika na Parole bila kujali aina na uzito wa makosa. Aidha, Sheria husika haikuanza kutumika mara moja kutokana na sababu zifuatazo:-

i.    Bodi ya Taifa ya Parole na Bodi za Parole za Mikoa zilizokuwa zimeundwa kwa mara ya kwanza zilivunjwa na kuundwa upya na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kulalamikiwa kuwa uteuzi wa Wajumbe wake haukuzingatia uwiano wa jinsia na dini.

ii.    Kutokamilika kwa maandalizi ya nyaraka mbalimbali muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Parole ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa semina kwa wajumbe wa Bodi za Parole za Mikoa yote nchini ili kufanikisha uanzishwaji na utekelezaji wa Sheria hiyo.

Baada ya matukio hayo, kikao cha kwanza cha Bodi ya Taifa ya     Parole kilifanyika tarehe 19 Agosti, 1999 ambacho kiliwajadili     wafungwa watano (5) na kupitisha watatu(3) walioonekana kutimiza     masharti ya kuachiliwa kwa Parole nchi nzima. Idadi hiyo ni ndogo     hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo magereza yote nchini     yalikadiriwa kuwa na wafungwa 27,000/=. Kutokana na wafungwa     hao watano waliojadiliwa, ilidhihirisha kuwa Sheria yenyewe ilikuwa     haitekelezeki kama ilivyokusudiwa katika mapendekezo     yaliyowasilishwa na Jeshi la Magereza hapo awali.

Matokeo haya yalisababisha Bodi ya Taifa ya Parole kuishauri     Serikali     kupanua wigo wa sheria hii ili wafungwa wengi zaidi     waweze     kunufaika. Mapendekezo haya yalilenga kifungu cha nne     cha sheria     ya Bodi za Parole vifungu vidogo (a),(b) na (c) ambavyo     vinataja     kuwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha,    waliofungwa kwa     makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha,     madawa ya kulevya,     kujamiiana na adhabu ya kifo iliyobadilishwa     kuwa kifungo kwamba     hawawezi kupata msamaha wa Parole.     Ilipendekezwa kwamba    kifungu hicho kirekebishwe ili     wafungwa wote wa makosa hayo nao     wafikiriwe kunufaika na     utaratibu wa Parole bila kujali makosa     waliyotenda.

Kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Parole, Sheria Na. 25/1994 ilifanyiwa marekebisho kwa Sheria     Na. 5/2002 ambayo ilijihusisha na eneo dogo tu kwamba badala ya mfungwa anayestahili Parole kuwa amehukumiwa kifungo cha miaka nane (8) na kuendelea, ilirekebishwa na kuwa awe amehukumiwa kifungo cha miaka minne (4) na kuendelea. Chini ya marekebisho hayo Wakili wa Serikali Mfawidhi wa kanda aliongezezwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Parole ya Mkoa. Hata hivyo suala la aina ya makosa na urefu wa kifungo katika kufikiriwa kunufaika kwa mpango wa Parole lilibaki kama lilivyokuwa hapo awali.
Baada ya marekebisho hayo ya Sheria ya Bodi za Parole, Bodi     za Parole za Taifa na Bodi za Mikoa zilizinduliwa upya mwaka 2003, na Bodi ya Taifa ya Parole ilifanya kikao chake cha kwanza mwezi Agosti, 2003     ambacho kilikuwa cha pili tangu Sheria hii ilipoanza kutumika rasmi nchini mwaka 1999.

3.0    MUUNDO WA BODI ZA PAROLE
Kwa mujibu wa Sheria ya Bodi za Parole (Cap 400 R.E 2002) kifungu cha 3(2)(a-d) na 3(4-9) Bodi zifuatazo ziliundwa ili kuhakikisha kuwa  Sheria ya Parole inatekelezeka hapa nchini.

3.1    Bodi ya Taifa ya Parole:

Bodi hii inaundwa na Wajumbe wafuatao:-
a)    Mwenyekiti wa Bodi ambaye huteuliwa na Mheshimiwa Rais.

b)    Wajumbe wawili ambao huteuliwa na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

c)    Wajumbe sita ambao huingia kwenye Bodi kutokana na nyadhifa zao.

Wajumbe hao ni:-
i).    Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) au Mwakilishi wake
ii).    Mganga Mkuu wa Serikali
iii).    Kamishna wa Ustawi wa Jamii
iv).    Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais
v).    Mkuu wa Jeshi la Polisi au mwakilishi wake
vi).    Mkuu wa Jeshi la Magereza ambaye ndiye Katibu wa Bodi

3.2    Bodi za Parole za Mikoa
Bodi za Parole za Mikoa zinaundwa na Wajumbe wafuatao:-
a)    Mwenyekiti wa Bodi ambaye huteuliwa na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

b)    Wajumbe wanne ambao huteuliwa na Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

c)    Wajumbe sita wanaoingia kwenye Bodi moja kwa moja kutokana na nyadhifa zao.
Wajumbe hao ni:-
i).    Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Kanda au mwakilishi wake
ii).    Mganga Mkuu wa Mkoa
iii).    Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa
iv).    Ofisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
v).    Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) au mwakilishi wake
vi).    Mkuu wa Magereza wa Mkoa (RPO) ambaye ndiye Katibu wa Bodi
Bodi hizi hudumu kwa kipindi cha miaka mitatu, baada ya hapo uteuzi mpya hufanyika.

4.0    SIFA ZA MFUNGWA WA PAROLE
Sheria ya Bodi za Parole Sura 400 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 1997 inaainisha kuwa mfungwa anayetumikia kifungo cha kuanzia miaka minne (4) na kuendelea anastahili kunufaika na mpango wa Parole kama atakuwa na sifa zifuatazo:-
i.    Asiwe amehukumiwa kifungo cha maisha

ii.    Asiwe ni mfungwa anayetumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa ya kulevya na makosa yanayohusiana na kujamiiana.

iii.    Asiwe ni mfungwa ambaye kifungo chake kimebatilishwa kutoka kwenye kifungo cha kunyongwa.

iv.    Awe anatumikia kifungo kisichopungua miaka minne (4) au zaidi na awe ametumikia 1/3 ya kifungo chake.

v.    Awe ameonesha tabia na mwenendo mzuri kwa muda wote aliokaa gerezani.

vi.    Asiwe na pingamizi la kimahakama la kukataliwa kunufaika  na utaratibu wa Parole chini ya Kifungu cha 67 cha Sheria ya makosa  ya Jinai.

5.0    UAMUZI BODI ZA PAROLE UNAVYOFANYIKA
Kimsingi mfungwa anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza hujulishwa kuhusu haki zake ikiwemo haki ya kuingizwa kwenye mpango wa Parole kama ana sifa kulingana na kosa lake na muda wa kifungo chake gerezani.  Mfungwa mwenye sifa ya kuingizwa kwenye mchakato wa Parole anapotimiza 1/3 ya kifungo chake, Afisa Parole hukusanya taarifa mbalimbali zinazomuwezesha kujadiliwa katika Bodi za Parole;  Taarifa hizo ni maoni kutoka kwa wazazi/ndugu zake, maoni ya mwathirika wa uhalifu, nakala ya hukumu, hati ya kifungo, maoni kutoka uongozi wa kijiji anachotarajia kwenda kuishi na maoni/taarifa kutoka kituo cha polisi kilichomkamata na pia matokeo ya uchunguzi wa alama zake za vidole kuhusu kumbukumbu zake za uhalifu.  Taarifa hizi zote huwa ni kwa ajili ya kudumisha usalama wa jamii na wa mfungwa mwenyewe anufaikapo kwa Parole.

Baada ya Taarifa hizi zote kukamilika kila mfungwa anayependekezwa kunufaika na Parole hufunguliwa jalada (Prison Form 64) kwa ajili ya kutunza kumbukumbu zake pamoja na taarifa za tabia na mwenendo wa mfungwa. Mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za Urekebishaji ya Gereza. Kamati hiyo hupitia taarifa hizo na kutoa maoni na mapendekezo kwenda Bodi ya Parole ya Mkoa.  Bodi ya Parole ya Mkoa hupitia maoni na mapendekezo hayo na baada ya uchambuzi wa kina, hutoa mapendekezo yake kwa Bodi ya Taifa ya Parole kupitia kwa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole.

Sekretarieti ya Taifa ya Parole ina jukumu la kuratibu shughuli za Bodi. Hivyo hupokea taarifa za wafungwa waliopendekezwa au kutopendekezwa kunufaika na Parole kutoka katika Bodi za mikoa. Huchambua taarifa hizo na kuandaa taarifa ya kila mfungwa kwa ajili kujadiliwa na Bodi ya Taifa ya Parole. Bodi hiyo kwa kutumia taaluma mbalimbali walizonazo wajumbe wake na nyadhifa zao hufanya uchambuzi wa kina wa mawasilisho hayo na kutoa uamuzi mfungwa anufaike au asinufaike na Parole. Uamuzi wa Bodi ya Taifa ya Parole huwasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Bodi za Parole Na 25 ya mwaka 1994 (Sura ya 400 R. E 2002). Mheshimiwa Waziri hupitia taarifa za kila mfungwa na kutoa uamuzi wa mwisho wa kukubaliwa au kukataliwa kunufaika kwa mpango wa parole. Uamuzi huo huwasilishwa kwa Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye ni Kamishna Jenerali wa Magereza.

6.0     MFUNGWA WA PAROLE ANAVYOTUMIKIA KIFUNGO CHINI YA UTARATIBU WA PAROLE
Baada ya maamuzi ya mwisho kutolewa na Mhe. Waziri, wafungwa waliokataliwa kunufaika na Parole huendelea kutumikia vifungo vyao, wale waliokubaliwa taarifa zao hutumwa katika magereza husika ili utaratibu wa kuwaachilia kwa Parole ufanyike. Kila mmoja hupewa kitambulisho (certificate) kitakachomtambulisha wakati wote akiwa kwenye Parole. Afisa Parole humpeleka mfungwa husika na kumkabidhi kwenye uongozi wa Serikali ya mtaa/kijiji kwa ajili ya ufuatiliaji wa tabia na mwenendo wa maisha yake ya kila siku. Uongozi wa kijiji/mtaa humteua mtu mmoja anayeheshimika katika jamii kuwa msimamizi wa mfungwa wa Parole, mfungwa wa Parole hutakiwa kutoa taarifa kwake kama atakavyokuwa amepangiwa. Afisa Parole kutoka katika gereza lililokaribu hutakiwa kumtembelea mfungwa husika kila mwezi na kuwasilisha taarifa kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole kwa ufuatiliaji.

Mfungwa wa Parole wakati wote wa Parole anatakiwa kufuata masharti aliyopewa na kutii Sheria za nchi na kuishi kwa amani wakati wote kama Sheria ya Bodi za Parole na Kanuni.  Masharti hayo yameainishwa sehemu ya 3 kanuni ya 5(5) (a-h). Inapotokea akivunja masharti ya Parole au kufanya uhalifu taarifa hupelekwa kituo cha Polisi na mfungwa hujulishwa kuhusu kusudio la kutengua Parole yake na ikithibitika tuhuma zilizotolewa dhidi yake ni za kweli hurudishwa gerezani na kufunguliwa mashtaka mapya na kupelekwa mahakamani, ikithibitika kweli amevunja masharti Mahakama ndiyo yenye uwezo wa kutengua Parole baada ya kumsikiliza kwa mujibu wa Kanuni ya Sheria ya Bodi za Parole za mwaka 1997 sehemu ya 5, 9(a-d) na Kanuni ya 10  (1-2). Aidha Mahakama inayo uwezo kutengua Parole kwa mfungwa yeyote na kuamuru arudishwe gerezani kama ikithibitika kwamba:-

i.    Amevunja sharti lolote la Parole

ii.    Baada ya kupata maombi kwa maandishi toka kwa Mhe. Waziri kwa maslahi ya Taifa kwa mujibu wa  Kanuni ya Sheria ya Bodi za Parole sehemu ya 5, 10(3) (a-c).

iii.    Kama mfungwa husika atafanya uhalifu akiwa kwenye Parole.
             
7.0    MAFANIKIO
Tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Bodi za Parole hapa nchi yapo mafanikio kadhaa ambayo yamepatikana kama ifuatavyo:-
(i)    Kuimarika kwa usalama ndani ya magereza nchini, hii inatokana na dhana kuwa ili mfungwa aweze kuingizwa kwenye mchakato wa Parole sifa mojawapo ni kuwa na mwenendo na tabia nzuri gerezani, hivyo wafungwa wa vifungo virefu magerezani waliokuwa wamekata tamaa au kukosa hamasa ya kuwa na nidhamu walirudishiwa matumaini kwa kigezo kuwa waweze kufikiriwa kuingizwa kwenye mchakato wa Parole, hivyo kusaidia kupungua kwa kiwango fulani cha tishio la usalama magerezani.

(ii)    Kuimarika kwa familia za wafungwa ambazo zilikumbwa na tishio la kusambaratika; Mfungwa anapotoka kwa Parole huenda kuishi kwenye jamii yake na kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo katika familia yake, huweza kusaidia familia yake hata kusomesha watoto  ambao wangeweza kukimbilia mitaani kujitafutia kipato baada ya mzazi/mlezi kufungwa gerezani kwa muda mrefu. Wafungwa WAFUATAO wameonesha mafanikio makubwa na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka wakiwa wanatumikia vifungo vyao chini ya Parole.  Mfano: Aliyekuwa mfungwa Na. 85’2008 Severine Paulo @ Supa wa kijiji cha Ovada, Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma alipotembelewa na Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole mwaka 2010 alikutwa anaendesha duka lililokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Tshs.3,000,000/=, shamba la mtama ekari 3, alizeti ekari 13 na ng’ombe (maksai) wawili (2) kwa ajili ya kilimo.

Aliyekuwa mfungwa namba 85/2006 Chacha Kerenge wa kijiji cha Mbirikili Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara alipotembelewa na Sekretarieti ya Bodi ya Parole ya Taifa Mwaka 2011, walimkuta anamiliki ng’ombe 30, mbuzi 166, na ekari 8 za shamba la mahindi, mali ambayo aliipata akiwa anatumikia kifungo nchini ya Parole. Wapo wafungwa wengine wengi ambao wakiwa wanatumikia vifungo chini ya Parole wameonesha maendeleo mazuri na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka.

(iii)     Tangu kuanzishwa kwa Sheria ya Bodi za Parole, Bodi ya Taifa ya Parole imeshakaa vikao 26 na katika vikao hivyo vyote wafungwa 4718 walikwishajadiliwa na wafungwa 4052 walinufaika kwa Parole;  Aidha, wafungwa 666 walikataliwa kutoka kwa Parole  kutokana na sababu mbalimbali.  Kati ya wafungwa hao walioachiliwa kwa Parole ni wafungwa 52 tu waliokiuka masharti na kurudishwa magerezani.  Dosari hii ni sawa na 1.3%, hii inaonesha kwamba adhabu mbadala ni muafaka katika mazingira ya leo.
(iv)    Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole na Sekretarieti yake walitembelea nchi ya jirani ya Zambia kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa Parole na uongozi wa magereza.

7.1    CHANGAMOTO
Katika kutekeleza Sheria ya Bodi za Parole changamoto mbalimbali zimejitokeza ambazo zimekuwa ni kikwazo katika utendaji wa shughuli za Parole kama ifuatavyo:-
(i)    Sheria ya Bodi za Parole kuwa na wigo finyu kiasi kwamba haiwanufaishi wafungwa wengi wenye vifungo virefu.  Pamoja na sheria hii kufanyiwa marekebisho kwa Sura 400 ya mwaka 2002 wafungwa wengi wanaotumikia vifungo virefu bado hawapati fursa ya kunufaika kwa kuwa aina ya makosa wanayotumikia yamezuiliwa na sheria hii.

(ii)    Uelewa mdogo kuhusu Parole miongoni mwa jamii (Public awareness).  Ushiriki wa jamii katika kumrekebisha mfungwa ni wa muhimu sana, ili jamii iweze kushiriki vizuri katika jambo hili zinahitajika juhudi za dhati katika kutoa elimu kuhusu Parole. Hasa kwa kuzingatia dhana kwamba uhalifu hufanyika kwenye jamii hivyo na urekebishaji wake ni muhimu ufanyike katika jamii husika.

(iii)    Wafungwa waliopo chini ya utaratibu wa Parole kukosa mitaji ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali pamoja na ugumu wa kupata ajira.  Mara nyingi wafungwa wanapotoka magerezani baada ya kukaa kwa muda mrefu hukuta familia zao zimetawanyika na hata mali zao kutapanywa ovyo, hivyo huhitaji msaada wa kuwezeshwa kuanza maisha upya.
(iv)    Mtizamo hasi wa jamii kuhusu mfungwa. Jamii inashindwa kutambua kwamba, mfungwa anapokuwa gerezani anapitia program mbalimbali za urekebishaji na hivyo anakuwa amerekebika. Badala yake, humnyanyapaa na kumnyooshea vidole na hata kushindwa kumpa ushirikiano ipasavyo.

8.0 MIKAKATI YA KUBORESHA PAROLE NCHINI
Kwa kuwa utekelezaji wa Sheria ya Bodi za Parole Tanzania Bara una changamoto nyingi, ipo mikakati mbalimbali inayofanywa na Bodi ya Taifa ya Parole kwa ajili ya kuimarisha na kuborehsa utaratibu wa Parole. Miongoni mwa mikakati hiyo ni:-

(i)    Kifungu cha nne (4) cha Sheria ya Bodi za Parole Na. 25/1994 iliyofanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 5/2002 bado inaonekana kuwa na mapungufu kwa sababu, wigo wa wafungwa wenye sifa za kunufaika na Parole ni mdogo ukilinganisha na idadi kubwa ya wafungwa wa vifungo virefu wanaokosa sifa kwa mujibu wa masharti yaliyoainishwa kisheria. Mapendekezo ya maboresho ya Sheria hiyo yanafanyiwa kazi. Lengo likiwa ni kupanua wigo ili wafungwa wenye makosa yaliyozuiliwa wapate fursa hiyo baada ya Kamati za urekebishaji pamoja na Bodi za Parole kujiridhisha kuwa amerekebika na siyo hatarisho kwa jamii anayotarajia kwenda kuishi nayo.

(ii)    Jeshi la Magereza ambalo ndiyo Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole linaendelea na utaratibu wa utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu Sheria ya Bodi za Parole kupitia Radio ya Taifa (TBC Taifa) kipindi kiitwacho "Ijue Magereza”. Sanjari na hatua hiyo, Sekretarieti inakamilisha maandalizi ya kutoa vipeperushi mbalimbali vitakavyoielimisha jamii kuhusu masuala ya mpango wa Parole. Katika jitihada za kuifanya jamii ipate uelewa zaidi kuhusu Sheria ya Bodi za Parole na utekelezaji wake.

(iii)    Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole ina mpango wa kuendesha semina maalumu kwa wadau mbalimbali ili kupata maoni yao kuhusu utekelezaji wa Sheria za Parole ili kuhamasisha ushiriki wa Jamii katika suala zima la kuongeza ufanisi katika utekelezaji. Aidha, kuendelea kuimarisha mahusiano ya karibu na Serikali za mitaa, vijiji na familia ambao ni wadau wakubwa katika kuwasimamia wafungwa wa Parole na kuwasaidia kujiunga na jamii.
(iv)    Bodi kutumia fursa ya vikao vyake mbalimbali kutafakari mustakabali wa programu ya Parole nchini ili kutoa maoni yatakayowezesha Taifa kuboresha programu hiyo siku hadi siku.
(v)    Wajumbe wa Bodi kutembelea magereza mbalimbali nchini kujionea mazingira wanayoishi wafungwa pamoja na kupata maoni yao kuhusu Parole.

9.0 HITIMISHO
Hakuna mtu anayezaliwa na tabia ya uhalifu. Jamii ndiyo inayomjengea mazingira ya kujifunza tabia hiyo. Hivyo basi, jamii inawajibika kubadili mazingira yake ili naye aweze kubadili tabia na kuishi kama raia mwema. Sanjari na marekebisho tajwa, juhudi maalumu zitaendelea kufanyika katika kuhakikisha suala zima la ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji wa Sheria ya Bodi za Parole linatiliwa mkazo inavyostahili.  Hasa ikizingatiwa kuwa jamii ina nafasi kubwa katika kumjengea mtu mazingira ya kujifunza tabia na mwenendo mzuri na kumwezesha kujirekebisha na kuachana na vitendo vya uhalifu.

.