MAJUKUMU YA KITENGO CHA AFYA, TIBA NA LISHE
UTANGULIZI:

Kitengo cha Afya, Tiba na Lishe kipo chini ya Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magerezda. Kwa mujibu wa muundo wa Jeshi la Magereza wa mwaka 2010, kitengo hicho kina majukumu yafuatayo:-

• Kusimamia upatikanaji na usimamizi wa dawa na vifaa tiba.
• Kuendesha elimu ya afya kwa watumishi na wafungwa.
• Kudhibiti mlipuko wa magonjwa Magerezani
• Kupendekeza wafungwa wanaotakiwa kuachiwa kwasababu za kiafya.
• Kusimamia ubora wa chakula Magerezani na kushauri ipasavyo.

MAFANIKIO YA KITENGO CHA AFYA, TIBA NA LISHE:
Kitengo cha Afya, Tiba na Lishe kimefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Mafanikio ya kitengo hiki yanatokana na ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Magereza na taasisi nyingine za Kiserikali na zisizo za Kiserikali. Baadhi ya taasisi zinazoshiriki katika kuboresha huduma za afya Magerezani ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mamlaka za Serikali za mitaa, Tume ya Kudhibiti UKIMWI, Shirika la Misaada la watu wa Marekani (USAID), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), PharmAccess Foundation, Vaasa Association For Developing Countries (VADC), New Life in Christ, Mildmay International.

Kupitia ushirikiano huo huduma za afya, miundo mbinu na huduma nyinginezo zimeboreshwa kama ifuatavyo:-

• Ukarabati na ujenzi wa Zahanati na vituo vya afya kwa Magereza ya Arusha, Wazo Hill, Keko, Ukonga, Segerea, Isanga, Iringa, Bukoba, Karanga, Lindi, Babati, Musoma, Ruanda, Mtego wa Simba, Lilungu, Butimba, Ubena, Songea, Kitai, Shinyanga, Singida, Uyui, Mahabusu Urambo, Maweni, Chuo Ukonga na Bwawani Sekondari.

• Mafunzo kwa wataalamu wa afya kuhusu utoaji wa huduma mbalimbali kama vile utoaji wa dawa za kufubaza makali ya UKIMWI, ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa hiari, Huduma za wagonjwa majumbani, matibabu kwa magonjwa ya ngono, huduma ya kuzuia Maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto, na huduma za Maabara.

• Kupatikana kwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya tiba na uchunguzi kama vile Digital X- Ray machine (Gereza Ukonga), Gene X- Pert machine (Gereza Ruanda, Ukonga, Keko, Segerea na Butimba), CD4 Machine (Gereza Ruanda, Segerea, Butimba na Chuo Ukonga), Haematology mashine, Urine Chemistry analyzer (Chuo Ukonga).

• Mafunzo ya elimu rika kuhusu UKIMWI kwa watumishi, familia za watumishi na wafungwa. Hii imesaidia kuongeza uelewa na kupunguza unyanyapaa.

• Ununuzi na usambazaji wa kondomu za kiume na za kike kwa ajili ya matumizi ya watumishi na wafungwa wanaomaliza vifungo.

• Kuimarika kwa mfumo wa uwekaji kumbukumbu za wagonjwa.

• Maafisa na askari wa Jeshi kupata uhakika wa matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

CHANGAMOTO:

Pamoja na mafanikio yaliyopo katika Kitengo cha Afya, Tiba na Lishe, zipo baadhi ya changamoto kama ifuatavyo:-
(i) Uhaba wa wataalamu unaotokana na wimbi kubwa la kuacha kazi kwa Maafisa na askari.
(ii) Uchakavu na ukosefu wa vifaa vya Maabara na vifaa tiba mbalimbali.
(iii) Kukosekana kwa magari ya kusafirishia wagonjwa (Ambulance).
(iv) Msongamano wa wafungwa Magerezani.
(v) Kukosa uwezo wa kuendeleza miradi baada ya wahisani kumaliza muda wao na kuondoka.
(vi) Kukosekana kwa hospitali yenye Madaktari Bingwa kwa ajili ya kuhudumia wafungwa, watumishi, Maafisa/askari wastaafu na familia za watumishi
(vii) Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutolipia baadhi ya huduma za matibabu.


Kwa miaka ya hivi karibuni huma za afya Magerezani zimeboresha kwa kiwango cha kuridhisha. Juhudi zaidi zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa na kuwezesha kupatikana kwa huduma bora kulingana na viwango vya Kitaifa na Kimataifa
.