VIWANDA VIDOGOVIDOGO
Kitengo cha viwanda vidogovidogo kipo chini ya divisheni ya Huduma za Urekebishaji. Malengo ya divisheni ya huduma za urekebishaji ni kuwarekebisha wafungwa kwa kuwapatia ujuzi kupitia nyanja za viwanda vidovidogo, kilimo na ujenzi ili kuwafanya kuwa watu wema na kutokurudia kutenda uhalifu na badala yake waweze kujiajiri wenyewe.
Kitengo cha viwanda kinahusika na usimamizi wa viwanda vidogovidogo vilivyopo chini ya Jeshi la Magereza. Baadhi ya viwanda hivi vinajiendesha kupitia Shirika la Magereza (Coorpation Sole) na vilivyobaki viko chini ya Serikali ambavyo hupokea fedha za uendeshaji toka Serikalini.

1. VIWANDA VINAVYOSIMAMIWA NA SHIRIKA LA MAGEREZA
a. Viwanda vya seremala (samani)
Viwanda hivi vipo gereza ukonga (DSM), gereza Arusha na gereza Uyui (Tabora). Viwanda hivi hutengeneza samani (furniture) kwa ajili ya matumizi ya ofisi na nyumba. Pia hupokea agizo mbalimbali kutoka Idara za Serikali, taasisi za Serikali na watu binafsi.

b. Kiwanda cha viatu
Kiwanda hiki kipo gereza Karanga Moshi(Kilimanjaro). Kiwanda hiki kinatengeneza aina mbalimbali za viatu, mikoba, mikanda, mikoba ya komputa mpakato, makasha ya kuwekea bastola na pochi za kuwekea fedha.

c. Viwanda vya ushonaji
Viwanda hivi vipo gereza Ukonga (DSM), Gereza Ruanda (Mbeya), gereza Butimba (Mwanza) na gereza Arusha. Viwanda hivi hutengeneza sare za askari wa Jeshi la Magereza, wafungwa na Idara nyingine za Serikali pamoja na sekta binafsi.

d. Kiwanda cha sabuni
Kiwanda hiki kipo gereza Ruanda (Mbeya), kiwanda hiki hutengeneza sabuni mbalimbali kama vile, sabuni za kufulia,kuogea na sabuni za chooni. Sabuni hizi hutumiwa na wafungwa na zinazobaki huuzwa katika soko huru.

e. Karakana
Karakana hizi zipo KPF (Morogoro) na Gereza Ukonga (DSM) Karakana ya KPF Morogoro inatengeneza majiko ya mkaa na majiko ya kutumia kuni. Majiko haya hutumika kwenye Magereza pamoja na watu binafsi. Karakana ya Ukonga inatarajiwa kuanza uzalishaji punde tu mara baada ya kumalizia ufungaji wa mashine.

f. Viwanda vya chumvi
Viwanda hivi vipo Mtwara na Gereza Kigongoni (Bagamoyo). Chumvi inayozalishwa katika viwanda hivi hutumika kwenye Magereza kwa ajili ya wafungwa na ile ya ziada huuzwa kwa watu binafsi.

2. VIWANDA VIDOGO VINAVYOENDESHWA KWA FEDHA ZA SERIKALI
a. Kazi za mikono
Viwanda vya kazi za mikono vipo gereza Ukonga (DSM), gereza Butimba (Mwanza), gereza Isanga (Dodoma), gereza Maweni (Tanga), gereza Lindi, gereza Mtwara, gereza Njombe, gereza Bangwe (Kigoma), gereza Karanga, (Moshi), gereza Ruanda (Mbeya), gereza KPF (Morogoro) na gereza Musoma (Mara). Shughuli za kazi mikono ni ushonaji, ufumaji, uchongaji na nyinginezo. Vifaa vinavyotengenezwa ni table mates, mazulia ya mlangoni, vikapu, masweta na vikoi. Bidhaa hizi huuzwa kwa watu binafsi katika maonesho ya Sabasaba na Nanenane.

b. Viwanda vya mafuta ya kupikia.
Hivi vipo vya aina mbili kutokana na aina ya mafuta yanayotengenezwa. Aina ya kwanza ni viwanda vya ukamuaji wa mafuta ya mawese ambavyo vipo gereza Kwitanga (Kigoma) na Kambi Kimbiji (Dar es Salaam) na aina ya pili ni kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti ambacho kipo gereza Ushora (Singida). Sehemu kubwa ya mafuta yanayozalishwa toka viwanda hivi hutumiwa na wafungwa waliopo katika Magereza mbalimbali na kiasi kinachobaki huuzwa katika soko huru.

c. Viwanda vya kokoto
Viwanda hivi vipo gereza Wazo Hill (DSM) gereza Msalato (DSM) na gereza Maweni (Tanga) kokoto zinazozalishwa huuzwa kwa watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi.

d. Kiwanda cha chumvi
Kiwanda hiki kipo gereza Lindi. Chumvi inayozalishwa kiwandani hapo hutumika gerezani kwa matumizi ya wafungwa na inayobaki kama ziada huuzwa kwa watu binafsi.

e. Kiwanda cha sabuni
Kiwanda hiki kipo gereza Ukonga (DSM). Sabuni zinazotengenezwa na kiwanda hicho hutumika kwa matumizi wafungwa.

f. Kiwanda cha mkonge
Kiwanda hiki kipo katika shamba la mkonge gereza Kihonda (Morogoro). Majani ya Mkonge huzalisha Singa za mkonge. Singa za mkonge zinazozalishwa huuzwa katika soko huria na nyingine hutumika kutengenezea mazulia ya mlangoni, “table mats”, vikapu na bidhaa mbalimbali.

g. Mashine za kusaga
Mashine hizi zipo gereza Bangwe (Kigoma), gereza Karanga (Kilimanjaro), gereza Arusha, gereza Mollo (Rukwa), Ofisi ya Mkuu wa Magereza (Shinyanga), gereza Ukonga (DSM) na gereza Babati (Manyara).

Jukumu la urekebishaji wa wafungwa kupitia kitengo cha viwanda vidogovidogo lina manufaa makubwa kwa Taifa letu, kwa mfungwa mwenyewe na jamii nzima kwa ujumla. Kama taifa, tunapata mapato kutokana na mauzo ya bidhaa zinazotengenezwa au kuzalishwa na pia, kuimarisha amani ya nchi yetu kutokana na mabadiliko ya tabia ya wafungwa kwani wamalizapo vifungo vyao hubadilika na kuwa raia wema wanaoishi kwa kufuata sheria za nchi.
.