DIVISHENI ZA HUDUMA YA UREKEBISHAJI |
1.0 UTANGULIZI Divisheni za Huduma ya Urekebishaji ni moja ya Divisheni tatu zinazounda Jeshi la Magereza. Divisheni zingine ni Divisheni ya Fedha na Utawala na Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magereza. Divisheni ya huduma za urekebishaji ndiyo mahsusi kwa urekebishaji wa tabia za wafungwa. Katika utekelezaji wa azma hii, Divisheni ya Huduma za Urekebishaji wa wafungwa imegawanyika katika vitengo vifuatavyo:- • Ujenzi na Ukarabati wa miundombinu • Kilimo, mifugo na hifadhi ya mazingira • Viwanda vidogovidogo. Katika vitengo hivi, wafungwa hufundishwa stadi mbalimbali za kazi ambapo hupata ujuzi mbalimbali kama vile ujenzi, shughuli za viwanda, kilimo, ufugaji bora na utunzaji wa mazingira. 1.1 UTEKELEZAJI Katika jitihada za kuboresha mazingira ya kazi zetu na kutekeleza jukumu la msingi la kurekebisha wafungwa divisheni hii imekuwa na kazi ya kutekeleza jukumu la msingi la kurekebisha wafungwa divisheni hii imekuwa na kazi mbalimbali kwa kila kitengo kama ifuatavyo:- 1.2 Ujenzi na Ukarabati Kitengo hiki kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa hufanya kazi za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya magereza kwa kuwashirikisha wafungwa pamoja na shughuli za ujenzi, kitengo hiki ndicho kinachosimamia na kuratibu masuala yote ya maendeleo ya ardhi iliyopo chini ya umiliki wa Jeshi la Magereza. Kitengo cha Ujenzi kina shughuli kuu zifuatazo:- i) Uimarishaji na upanuzi wa magereza ya zamani; ii) Ujenzi wa magereza mapya; iii) Ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Magereza wa Mikoa; iv) Ujenzi na ukarabati wa nyumba za askari; v) Ukarabati na ujenzi wa mifumo ya umeme, maji safi na maji taka; vi) Upimaji wa maeneo ya Magereza na kusimamia miongozo ya ardhi iliyopo chini ya Jeshi la Magereza. Pamoja na kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya Jeshi la Magereza, Kikosi hiki pia hufanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi na umeme kwa kujenga au kukarabati majengo ya Idara mbalimbali za Serikali, Mashirika na Watu Binafsi. Katika utekelezaji wake, Kikosi cha Ujenzi huwashirikisha wafungwa ikiwa ni sehemu mojawapo ya urekebishaji kwa kuwafundisha kwa vitendo stadi mbalimbali za ufundi kama vile uashi, umeme, useremala, ufundi rangi, bomba n.k ili wamalizapo vifungo vyao waweze kuutumia ujuzi huo katika jamii kwa kuwapatia kipato. 1.3.0 Kilimo, Mifugo na Utunzaji Mazingira 1. Jeshi la Magereza lina eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 130,482 ambalo hutumika kwa shughuli za Kilimo, Mifugo na Hifadhi ya Mazingira. Juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuhakikisha kuwa kilimo kwenye Magereza yetu kinakuwa cha kisasa na chenye tija, lengo kubwa likiwa ni kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na ziada kuuzwa kwa wananchi wengine. Aidha, mashamba haya pia yameendelea kuwa mashamba darasa ya kujifunzia kilimo kama mbinu mojawapo ya urekebishaji wa wafungwa. 2. Kwa sasa yapo mashamba makubwa 43 ambayo yamegawanyika kama ifuatavyo:- • Mashamba ya kilimo – 14 (Idete, Ludewa, Kwitanga, Kibiti, Mkwaya, Kimbiji, Pawaga, Kitete, Kalila, Mng’aro, Bagamoyo, Kihonda, Ngwala na Mang’ola; • Kilimo na Mifugo (Mixed farms) – 16 (Songwe, Arusha, Mollo, Butundwe, Kitai, Ilagala, Kibondo, Nachingwea, Wami Kuu, Kiberege, Ushora, Msalato, Kilimo Urambo, Kitengule, Isupilo na Kiabakari; • Ranchi za Mifugo – 11 (Mugumu, Mbigiri, KPF, King’ang’a, Namajani, Maji – Maji, Ubena, Rusumo, Kilwa na Kingurungundwa na Mollo; • Mashamba ya ng’ombe wa maziwa – 2 (Isupilo & KPF). Kati ya mashamba haya 43; mashamba 15 ya kilimo na mifugo yanaendeshwa na Shirika la Magereza kwa mpango wa “Revolving Fund”. Mashamba 28 yaliyobaki yanaendeshwa chini ya utaratibu wa Serikali, ambapo Serikali Kuu hutoa fedha za kuhudumia uzalishaji. Mazao yanayolimwa katika mashamba haya huuzwa na fedha kuingizwa Serikalini kama maduhuli. Mazao yanayozalishwa katika mashamba ya Magereza ni pamoja na mahindi, mpunga, maharage, mtama, mbegu za mafuta (Michikichi, Alizeti, Karanga, Ufuta) na uendelezaji wa bustani za mboga mboga za aina mbalimbali na matunda. Pia Jeshi linaendelea kutunza mashamba ya mazao mengine ya kudumu yakiwepo chai, mkonge, kahawa, minazi, korosho na miwa ambayo yapo katika Mikoa mbalimbali. Aidha, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika (Wakala wa Mbegu za Kilimo) ASA, pamoja na Makampuni ya Highland Seed Growers na TANSEED International, Jeshi la Magereza pia huzalisha mbegu za mazao ya kilimo zikiwepo mahindi, maharage, mpunga, mtama, kunde, choroko, ufuta, karanga, alizeti, mbegu mbalimbali za mboga mboga na vipando bora vya mihogo. Kwa upande wa mifugo, Jeshi la Magereza linaendeleza juhudi za ufugaji bora wa ng’ombe wa nyama na maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku na bata kwa kutumia teknolojia rahisi na za kisasa ili kuwa mfano wa kuigwa. Uvuvi: Kwa upande wa uvuvi, miradi huendeshwa katika maeneo yaliyo karibu na maziwa kama Butimba – Mwanza na Bangwe Kigoma. Aidha, ufugaji wa samaki unaendelea katika Magereza ya Karanga, Moshi, Kwamngumi – Tanga na jitihada zipo za kufufua/ kuanzisha ufugaji huo katika maeneo mengine pia. Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabia Nchi, Jeshi la Magereza huendesha shughuli zake kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira. Miti takribani 6,000,000 imeshapandwa katika eneo la jumla ya hekta 3526 katika Magereza mbalimbali nchini. Aidha, uoto wa misitu ya asili iliyopo katika maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza inayokadiriwa kufikia hekta 14,053 inaendelezwa kwa kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama. Miradi ya ufugaji nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta imeanzishwa na inaendelezwa katika kuhakikisha kuwa Jeshi linapata faida kubwa katika miradi ya utunzaji wa mazingira. 1.4 Viwanda vidogovidogo Kitengo cha viwanda kinahusika na kuwafundisha Wafungwa Stadi mbalimbali za ufundi kama seremala, ushonaji, utengenezaji wa sabuni, utengenezaji wa vifaa vya mikono (ufumaji, useketaji, uchoraji, ufinyanzi na ususi) kwa nia ya kuwarekebisha tabia ili wamalizapo adhabu zao wawe raia wema wanaoweza kujitegemea. Aidha, lengo kuu la Kitengo hiki ni kusimamia na kudhibiti uzalishaji bora wa bidhaa, kuandaa mfumo mzima wa maendeleo ya Viwanda vidogo vidogo na utekelezaji wake. Program za urekebishaji katika viwanda hutekelezwa na Wakuu wa Magereza/Viwanda kwa kushirikiana na Ofisi ya Makao Makuu. |
. |