HUDUMA ZA MAGEREZA
1. Utangulizi

Majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ni kuwapokea na kuwahifadhi gerezani watu wote wanaoletwa gerezani kwa mujibu wa sheria za nchi na kuendesha program mbalimbali zenye kulenga kuwarekebisha wafungwa waliohukumiwa ili hatimaye watoke gerezani wakiwa raia wema. Katika kutekeleza majukumu hayo Jeshi la Magereza linawajibika kufuata na kuheshimu sheria zote za nchi pamoja na sheria mbalimbali za kimataifa zinazohusu haki za binadamu.

Lengo la waraka huu wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni kuwaelimisha wateja wote wanaokuwa na mahusiano na chombo hiki kuhusu mambo yafuatayo:-

(i) Huduma zinazotolewa na chombo hiki kwa mujibu wa sheria na taratibu.
(ii) Wajibu wa chombo hiki kwa wateja wa aina zote.
(iii) Wajibu wa wateja wa aina zote katika mahusiano yao na chombo hiki.
(iv) Namna ya kutoa malalamiko pale mteja anapoona hakutendewa haki ipasavyo na chombo hiki.

2. Wateja wanaolengwa na Waraka huu

Wateja wanaolengwa na waraka huu ni:-

• Wafungwa wa aina zote wanaoingia magerezani

• Ndugu/jamaa za wafungwa

• Mawakili/wanasheria wa wafungwa

• Watu wanaotoa huduma mbali mbali kwa wafungwa, kama vile NGOs, madhehebu ya dini n.k.
• Wawakilishi/mabalozi wan chi mbalimbali hapa nchini pale wanapokuwa na wafungwa raia wan chi zao magerezani.

3. Haki za wateja
(i) Wafungwa na Mahabusu
• Mfungwa/Mahabusu anapopokelewa gereza kwa mara ya kwanza anayo haki ya kusomewa taratibu na sheria za magereza zitakazomuongoza awapo gerezani.
• Anayo haki ya kuyaeleza matatizo yake kwa uongozi wa gereza.
• Haki ya kupatiwa chakula kulingana na matakwa ya madhehebu yake.
• Haki ya kutembelewa na wakili wake wakati wowote na muda wowote.
• Haki ya kutembelewa na ndugu/jamaa zake wakati wowote awapo mgonjwa.
• Haki ya kutembelewa na Polisi, lakini mfungwa akubali kuonana naye na kwa madhumuni maalum.
• Mfungwa/mahabusu ambaye ni raia wan chi nyingine anapopokelewa gerezani anayo haki ya kupelekewa taarifa za kuwepo kwake gerezani kwa mwakilishi/balozi wan chi yake aliyepo nchini.
• Wafungwa wanayo haki ya kutembelewa na watu wasiozidi wawili kama mara moja kwa mwezi kwa muda wa dakika 15 au zaidi kwa kibali cha Mkuu wa Gereza na kwa nyakati zifuatazo:-
- Anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza
- Kabla ya kuhamishiwa gereza jingine
- Wakati ni mgonjwa mahututi
- Wakati wowote kwa kibali cha Mkuu wa Gereza kama vile atakavyoona inafaa.
• Haki ya kutembelewa na wakuu wa dini kwa ajili ya ibada kulingana na madhehebu yake.
• Haki ya kuandika au kupokea barua mara mbali kwa mwezi na kwa nyakati zifuatazo:-

- Anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza

- Anapoingia gerezani toka uhamisho

- Wakati wa kifo au ugonjwa wa ndugu au jirani yake.

- Wakati anapopatwa na shida za dharula za kifamilia n.k.

- Wakati atakapotaka kufanya mipango ya kazi au msaada baada ya kumaliza kifungo.

Barua zote zinazotoka na kuingia gerezani ni sharti zisanifiwe au kupitishwa na Mkuu wa Gereza.
• Haki ya kutia sahii nyaraka kwa mfano hundi, wosia n.k.
• Haki ya kujiendeleza na masomo ya juu kulingana na sifa zake za awali kitaaluma.
• Haki ya kupata huduma ya malazi na chakula kwa viwango vilivyowekwa na Serikali.
• Haki ya kupata huduma ya tiba na afya kwa ujumla.

(ii) Ndugu na Jamaa za Wafungwa
• Ndugu au jamaa yeyote wa mfungwa anayo haki ya kumtembelea mfungwa awapo gerezani kama ilivyoelezwa katika 3(i) hapo juu. Utaratibu wa kuwatembelea wafungwa ni kama ifuatavyo:- Jumamosi saa 6 mchana hadi saa 11 jioni, Jumapili saa 2 asubuhi hadi saa 6 mchana na saa 8 mchana hadi saa 10 jioni.

• Anayo haki ya kumwandikia mfungwa barua mara mbili kwa mwezi na kwa nyakati zilizoainishwa katika kipengele cha 3(i) hapo juu.


• Anayo haki ya kumpatia mfungwa huduma ya dawa za binadamu ambazo kwa wakati huo hazipo gerezani, baada ya kuidhinishwa na Daktari wa Serikali na kasha Mkuu wa Gereza husika kutoa kibali baada ya kufanya mawasiliano na Mganga wa Gereza.

• Anayo haki ya kumpatia mahabusu huduma ya chakula wakati wote awapo gerezani ili mradi amwarifu Mkuu wa Gereza ili amwondoe mahabusu mhusika kwenye orodha ya wale wanaopata huduma ya chakula kwa gharama ya serikali.

• Anayo haki ya kumpelekea mfungwa gerezani vifaa kama vile nyembe, dawa ya meno, miswaki, sabuni n.k ili mradi aombe na kupewa kibali na Mkuu wa Gereza husika.

(iii) Mawakili/Wanasheria wa wafungwa

• Wanayo haki ya kuwatembelea wafungwa au mahabusu wanaowawakilisha siku yoyote na wakati wowote. Suala la usiri wa mawasiliano baina ya wakili/mwanasheria na mfungwa/mahabusu ambaye ni mteja wao litaheshimiwa.

(iv) Watoa huduma wengineo

• Wanayohaki ya kuwapatia wafungwa huduma za kiroho wawapo gerezani kulingana na madhehebu yao baada ya kiongozi wa dhehebu husika kuomba na kupata kibali hicho sharti yapitishwe na Mkuu wa Gereza na Mkuu wa Magereza wa Mkoa.

• Wanayo haki ya kuwapatia wafungwa waliopo gerezani (kama ni shirika) huduma ya vifaa mbalimbali kama sabuni, mablanketi, nguo, chakula, madawa ya binadamu n.k ili mradi wawe wametuma maombi yao kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye atatoa kibali cha kuwaruhusu kutoa huduma hiyo. Wanaokusudiwa kupeleka mahitaji/msaada huo katika gereza husika kwa wakati huo.

• Wanayo haki ya kupatiwa wafungwa huduma za kisheria kwa kuwasiliana na Mkuu wa Gereza husika pamoja na Wakili kwa sharti kwamba awe Yule aliyechaguliwa/kukubalika na mteja mwenyewe.

(v) Wawakilishi/Mabalozi wan chi mbalimbali hapa nchini

• Wanayo haki ya kupatiwa taarifa za kuwepo gerezani kwa wafungwa raia wan chi zao.

• Wanapokuwa na wafungwa raia wan chi zao magerezani, wanayo haki ya kuwatembelea wakati wowote wanapoomba kufanya hivyo kwa kutuma maombi maalum kwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

• Wanayo haki ya kuwapa misaada ya hali na mali wafungwa/mahabusu raia wan chi zao waliopo magerezani, kwa mujibu wa sheria na taratibu.

4. Wajibu wa wateja
(i) Wafungwa/mahabusu

• Wafungwa na mahabusu wanawajibika kutii na kuheshimu sheria za Magereza na taratibu kuu zinazoendesha magereza wakati wote wa kuwapo kwao magerezani.
• Mfungwa hatapatikana na hatia ya kosa lolote la kinidhamu gerezani mpaka awe amepata nafasi ya kusomewa shitaka dhidi yake na kupewa nafasi ya kujitetea. Atapewa nafasi ya kuita mashahidi na pia kuhoji shahidi yeyote atakayeitwa na mashtaka yataendeshwa wakati yeye mwenyewe akiwepo.
• Wafungwa wanapaswa kuepuka kutenda makosa yaliyoorodheshwa chin ya Kanuni za Magereza (Makosa ya Wafungwa) za mwaka 1968

(ii) Ndugu/Jamaa za Wafungwa

• Ndugu au jamaa za wafungwa wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba wanatii taratibu zote zinazowahusu wafungwa wanapowatembelea gerezani, na hawatakiwi kuingiza vitu au vifaa vyovyote vilivyokatazwa kisheria. Kila gereza nchini litakuwa na tangazo maalum nje ya gereza likieleza sheria na taratibu zote zinazowahusu raia wote kuhusiana na Magereza na adhabu kutokana na ukiukwaji wa sheria na taratibu hizo.

(iii) Waatoa Huduma wengineo
Watoa huduma wengineo wanapaswa kuzingatia taratibu zote zilizoainisha kwenye 4(ii) hapo juu ama watakazoelekezwa na viongozi mbalimbali wa Magereza kuhusu taratibu za kufuata wanapotoa huduma za kibinadamu, hali na mali kwa wafungwa waliopo magerezani.

(iv) Mawakili/Wanasheria wa Wafungwa
Mawakili/Wanasheria wanawajibika kuzingatia taratibu zote zinazohusu kutembelea wafungwa magerezani kama zilivyoelezwa kwenye 4(ii) hapo juu. Vile vile wanapaswa kuzingatia kwamba mashauri yote yanayohusu wafungwa wanawashughulikia kisheria ni sharti yaanze kwa Mkuu wa Gereza husika.

(v) Wawakilishi/Mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini
Wanawajibika kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia suala la kuwatembelea raia wa nchi zao waliopo gerezani kama watakavyoelekezwa na ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza pale wanapofuatilia kibali cha kwenda gerezani.


5. Mteja asiporidhika
(i) Wafungwa/Mahabusu

• Iwapo mfungwa atapatikana na hatia ya kosa kubwa mbele ya Mkuu wa Gereza, kama anataka anaweza kuomba shauri lake lirudiwe na Kamishna Jenerali wa Magereza akieleza sababu za kutoridhika na uamuzi huo ambapo ataandika barua na kuipitisha kwa Mkuu wa Gereza, na Mkuu wa Magereza wa Mkoa alipo mfungwa huo.

• Kama ametendewa jambo ambalo anadhani siyo sahihi ataandika barua kwenda kwa Kamishna Jenerali wa Magereza kupitia kwa Mkuu wa Gereza na Mkuu wa Magereza wa Mkoa husika.

(ii) Ndugu/jamaa za wafungwa
Wakiona kwamba hawakutendewa haki kwa mujibu wa sheria na taratibu wapeleke malalamiko yao kwa Mkuu wa Gereza husika.

Wasiporidhika na hatua za Mkuu wa Gereza wapeleke malalamiko kwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa husika. Wasiporidhika kwenye ngazi hiyo wawasiliane na Ofisi ya Mkuu wa Magereza.


(iii) Mawakili/wanasheria wa Wafungwa

Wasiporidhika na huduma wanaweza kulalamika kwa Mkuu wa Gereza husika, Mkuu wa Magereza wa Mkoa husika hadi kwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

(v) Watoa Huduma wengineo

Wakiwa na malalamiko dhidi ya huduma watapitia ngazi za Mkuu wa Gereza, Mkuu wa Magereza wa Mikoa husika hadi kwa Kamishna Jenerali wa Magereza.
(vi) Mabalozi/wawakilishi wa nchi za nje
Watawasilisha malalamiko yao moja kwa moja kwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

6. Ngazi zaidi za kupeleka malalamiko

Iwapo mteja yeyote atakuwa hakuridhika na hatua zilizochukuliwa kushughulikia malalamiko yake dhidi ya huduma za Jeshi la Magereza hata baada ya kufikia ngazi ya Kamishna Jenerali atapeleka malalamiko yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Iwapo malalamiko yake yanahusu haki za binadamu na hakuridhika na hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi atawasilisha malalamiko yake kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
.